Mwanamke akatwa titi na mkono na mumewe kwa kufuta 'missed call' kwa simu

Mumewe alitaka kuona namba iliyopigwa siku mbili zilizopita ilipokosekana ndio akamshambulia vikali kwa upanga.

Muhtasari

• Mwathirika alisema kwamab baada ya kula mumewe alimtaka kumuonesha namba zote zilizopigwa kwa simu yake.

• Alipopata hakuna, ndio alimshambulia kwa upanga katika kile kilichoonekana kama ni kumshuku kimapenzi.

Maria Marwa, aliyekatwa titi na mkono na mumewe
Maria Marwa, aliyekatwa titi na mkono na mumewe
Image: Azam Tv

Polisi wanaendelea kumsaka kwa udi na amabari mwanaume mmoja anayetuhumiwa kumkata mkewe titi moja na mkono kwa kutumia panga.

 

Tukio hilo limeripotiwa katika nchi Jirani ya Tanzania ambapo mwathirika Maria Marwa alikatwa na mumewe Warema Wambura kwa upanga katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

 

Maria alieleza kwamba mumewe alizua zogo baada ya kutaka kuiona meseji ya simu iliyopigwa na ikakosekana kuchukuliwa, almaarufu missed call kwa kimombo, meseji hiyo ilikosekana na mwanaume huyo akaanzisha fujo na kumkata mkewe mkono na titi moja.

 

Runinga ya Azam iliripoti kwamba wawili hao walikuwa wamedumu katika ndoa kwa miaka 19 na tukio hilo lisilo la kawaida lilitokea pindi tu baada ya chakula cha jioni, Werema Wambura, alimuuliza moja ya namba ya simu iliyopigwa siku mbili zilizopita katika simu yake (Maria), lakini Maria alimjibu, hakuna namba yoyote.

 

Jibu hilo lilimpandisha hasira mithiri ya mkizi ambapo alikimbilia panga na kunyofoa titi lake la kushoto pamoja pia na mkono, tukio ambalo sasa limemuacha mkewe na ulemavu wa kudumu.

 

“Tulikuwa tumemaliza kupika, tukaenda kulala akaniambia amka nenda niletee simu yangu na unipekulia majina yote, nikafanya hivyo. Akaniuliza kuna namba moja iliyopigwa juzi iko wapi missed call, nikamwamia mimi sijui nimeshafuta. Hapo ndio alitoka kitandani na kuchukua panga mfunguni na kuanza kunishambulia,” mwathiriwa alielezea akiwa katika kitanda cha hospitali.

 

Aidha alisema sio mara ya kwanza kupigwa kwani mwaka 2016 alimpiga hadi kulazwa hospitali ambapo ugomvi ulisuluhishwa na waliendelea kuishi pamoja.

 

Kwa upande wake Daktari amesema kuna sehemu ya mkono wa Maria ilianza kuharibika hivyo walilazimika kuikata lakini pia majeraha mbalimbali wameyatibu kwa kuyashona na sasa anaendelea vizuri.