Korea Kaskazini yarusha kombora Japan

Kombora hilo lilianguka katika Bahari ya Pasifiki yapata kilomita 3,000 kutoka Japan.

Muhtasari

•Korea Kaskazini imerusha kombora linaloshukiwa kuwa la masafa ya kati katika sehemu ya kaskazini mwa Japan.

•Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida alilaani vikali vitendo hivyo, akielezea uzinduzi huo kama "tabia ya ukatili"

Habari za Korea Kaskazini zilisema kwamba Kim Jong-un alikuwa ameamuru kurusha makombora zaidi katika eneo la Pacific
Image: BBC

Korea Kaskazini imerusha kombora linaloshukiwa kuwa la masafa ya kati katika sehemu ya kaskazini mwa Japan.

Ilisababisha onyo kutoka kwa serikali ya Japan kwa watu katika kisiwa cha Hokkaido kujificha wakati wa wa kurushwa kwa kombora hilo, na kusimamishwa kwa muda kwa shughuli za treni.

Ni mara ya kwanza kurusha kombora la Korea Kaskazini juu ya Japan tangu 2017. Umoja wa Mataifa umepiga marufuku Korea Kaskazini kufanya majaribio ya silaha za makombora na nyuklia.

"Korea Kaskazini inaonekana kufyatua kombora. Tafadhali ondokeni kwenye majengo au chini ya ardhi," serikali ya Japani ilisema katika tahadhari ya dharura iliyotolewa saa 07:29 saa za ndani siku ya Jumanne (22:29 GMT Jumatatu).

Maafisa walisema kuwa kombora hilo lilianguka katika Bahari ya Pasifiki yapata kilomita 3,000 kutoka Japan, na kwamba hakuna majeraha yoyote yaliyoripotiwa kuhusiana na hilo.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida alilaani vikali vitendo hivyo, akielezea uzinduzi huo kama "tabia ya ukatili", na serikali ya Japan imeitisha mkutano wa Baraza lake la Usalama la Kitaifa.

Uzinduzi huo unaonekana kuwa ni ongezeko la kimakusudi lililoundwa ili kuvutia hisia za Japan na Marekani, ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakimpuuza kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.

Ni kinyume kabisa na kanuni za kimataifa kurusha makombora kuelekea au juu ya nchi nyingine bila ya onyo la awali au mashauriano.

Nchi nyingi huepuka kufanya hivyo kabisa kwani inaweza kudhaniwa kuwa ni shambulizi, na ingawa sio kubwa kama jaribio la nyuklia - ambalo linaweza kufuatiwa - hata hivyo linachochea sana.

Marekani imejibu, huku mwanadiplomasia mkuu wa Marekani katika eneo la Asia Mashariki, Daniel Kritenbrink, akielezea uamuzi wa Korea Kaskazini kuwa "wa bahati mbaya".

Haya yanajiri wakati Japan, Marekani na Korea Kusini zilifanya mazoezi ya kijeshi ya pande tatu mapema wiki iliyopita, ambayo yamejulikana kuichokoza Pyongyang.

Urushaji wa kombora hilo ni wa tano kutekelezwa na Pyongyang katika kipindi cha wiki moja.

Siku ya Jumamosi, roketi mbili zilianguka kwenye maji nje ya eneo la kipekee la kiuchumi la Japan.

Majaribio mengi ya makombora ya Korea Kaskazini hufanywa kwenye anga la juu, kuepuka njia za ndege juu ya majirani zake. Lakini kurusha juu katika anga la Japani kuliwaruhusu wanasayansi wa Korea Kaskazini kufanya majaribio ya makombora chini na "ambayo ni fursa nzuri zaidi ya majaribio na itawapatia majibu sahihi kama wangetumia kushambulia nchi", mchambuzi Ankit Panda aliambia shirika la habari la Reuters.

Mapema mwezi huu, Korea Kaskazini ilipitisha sheria iliyojitangaza kuwa taifa la silaha za nyuklia, huku kiongozi Kim Jong-un akifutilia mbali uwezekano wa mazungumzo ya kutokomeza silaha za nyuklia.Pyongyang ilifanya majaribio sita ya nyuklia kati ya 2006 na 2017, licha ya vikwazo vingi.