• Uganda itakuwa inasherehekea siku yao ya uhuru kwa kutimu miaka 60 Jumapili, Oktoba 9.
•Ziara yake Ruto itakuwa ya kuzima mgogoro wa kidipomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amemwalika Rais William Ruto kwa sherehe za kuadhimisha Uhuru wa taifa hilo Oktoba 9 kwa kile kinachoaminika kuzima moto uliyokuwa umeashwa na mwanawe Museveni Muhoozi Kainerugaba.
Rais Ruto atakuwa miongoni mwa viongozi walioalikwa na Rais Museveni kuadhimisha miaka 60 tangu Uganda ipate uhuru. Rais Ruto anatarajiwa kuondoka Jumamosi, Oktoba 8 kuhudhuria sherehe hiyo.
Baadhi ya wananchi wanahisi kuwa ziara ya Ruto itakuwa ya kuzima moto wa kichini chini uliyokuwa umewasha na matamshi ya kejeli dhidi ya Kenya na baada ya Mwanawe Rais Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye alidai kwamba itamchukua chini ya wiki mbili kutwaa jiji la Nairobi.
Jambo ambalo lilizua mjadala mkali miongoni mwa wakenya wakisema matamshi hayo ni ya kudunisha Kenya na yanafaa kuchukuliwa kwa uzito.
Maneno hayo ya Muhoozi, yalimfanya Rais Museveni kuomba msamaha kwa Wakenya kwa niaba ya mwanawe.
Msamaha wa Museveni ambaye ametawala Uganda kwa takribani miaka 36, ulionekana kama Rais mwenye kustawisha undugu wa mataifa hayo mawili.
"Ndugu zangu Waganda, ndugu zangu wa Wakenya, na wana Afrika Mashariki wote. Nawasalimu nyote. Nawaomba ndugu zetu wakenya watusamehe kwa maneno yaliotumwa na Jenerali Muhoozi," Museveni alisema.