Miili ya watoto 11 vipofu walioungua moto shuleni yakabidhiwa familia zao

Wiki moja iliyopita taarifa za moto kuchoma mabweni ya shule ya watoto walemavu wa macho Uganda zilivunja mioyo ya watu.

Muhtasari

• Gari la kubeba maiti lilizuka katika ua la shule hiyo Jumatano asubuhi na majeneza kutolewa ndani moja hadi kumi na moja, yote yakiwa na miili ya watoto hao.

Majeneza yaliyobeba mabaki ya miili ya watoto walioaga dunia
Majeneza yaliyobeba mabaki ya miili ya watoto walioaga dunia
Image: Maktaba

Wiki jana, taifa la Uganda liligubikwa na majonzi baada ya taarifa kuripoti kuwa moto ulizuka katika shule ya watoto walemavu wa macho.

Noto huo uliripotiwa kuwaunguza watoto vipofu 11 hadi kuwa majivu katika shule ya watoto walemavu wa macho kwa jina Salama iliyopo eneo la Mukono.

Jarida la Daily Monitor Alhamisi asubuhi liliripoti kuwa mamia ya watu walifurika katika uwanja wa shule hiyo Jumatano kupokea miili ya watoto hao 11 walioangamia katika mkasa mbaya wa moto.

“Gari la kubeba maiti lenye ukubwa wa kiasi cha haja lilipandishwa hadi kwenye eneo la Shule ya Wasioona ya Salama. Na wachukuzi wakashuka, na jeneza mkononi. Kisha wakatoa majeneza, si moja au mawili bali 11. Kila moja iliviringishwa ndani ya hema jeupe lililozungukwa na magurudumu nane. Ndani ya majeneza madogo 11 meeupe kulikuwa na mabaki ya wanafunzi vipofu ambao waliangamia kwenye moto huo,” Daily Monitor walihadithia kwa majonzi makubwa.

Marehemu wote waliteketea kwa moto kiasi cha kutotambulika kwa hiyo serikali ililazimika kuwafanyia vipimo vya DNA ili kujua ni nani aliyesalia kabla ya kukusanya familia zilizokuwa na huzuni Jumatano kuwapokea.

Watu mbali mbali waliokuwa wameguswa na msiba huo walijumuika katika ua la shule hiyo tangia alfajiri pasi na kujali hali mbaya ya anga ambayo ilikuwa ya manyunyu na kijibaridi shadidi.

Pindi tu miili hiyo ilipowasili, jarida hilo linaeleza kwamba waombolezaji walishindwa kujizuia huku kila mmoja akitokwa na kwi kwi za vilio.

“Maumivu na uchungu wa vifo hivyo jana vilidhihirika katika msukosuko wa kihemko ambapo zaidi ya jamaa na wakaazi, wanahabari waliokuwa wakiripoti misa hiyo pia walivunjika. Wazazi na walezi wengi walianguka, jambo ambalo lilisababisha watu wenye mapenzi mema kuwapepea kwa vitambaa,” Jarida hilo lilinakili.