Uganda: Maafisa wa serikali wakamatwa kwa kuiba chakula cha msaada dhidi ya Ebola

Maafisa hao wawili akiwemo chifu walisemekana kuiba takribani kilo 1100 za unga wa mahindi uliotolewa kuwasaidia watu walioathirika kwa kufungiwa kutotoka.

Muhtasari

• Mwanzoni walisema chakula hicho kilikuwa mikono salama ila baada ya uchunguzi ikagundulika chakuja hicho kimetoweka kwa njia tata.

Polisi Uganda wamewakamata wezi wa chakula cha msaada
Polisi Uganda wamewakamata wezi wa chakula cha msaada
Image: Facebook, Daily Monitor

Mamlaka ya polisi nchini Uganda imewakamata wafanyikazi kadhaa wa serikali baada ya kutuhumiwa kwa kuiba chakula cha msaada kilichotolewa kwa wahanga wa ugonjwa wa Ebola.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa na gazeti la Daily Monitor, watatu hao wanatuhumiwa kwa kuiba zaidi ya tani 1.1 za unga wa mahindi uliokuwa umetolewa ili kuwasitiri waathirika wa ugonjwa wa Ebola ambao unazidi kupenya katika maeneo mengi ya taifa hilo linalopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako ndiko chimbuko na ugonjwa huo kwa miaka mingi.

Polisi kutoka kituo cha Kassanda walidhibitisha kukamatwa kwa watatu hao ambapo mmoja ni mwenyekiti wa kaunti ndogo ya Nalutuntu, wa pili ni chifu na wa tatu akiwa ni afisa wa kitengo cha usalama wa ndani.

Jarida hilo lilieleza kuwa chakula cha msaada kilichoibwa kilikuwa kinaenda kuwanusuru wananchi waliokuwa wameathirika kutokana na kafyu iliyowekwa sehemu hiyo ya Nalutuntu.

“Kukamatwa kwa watatu hao kulifuatia kutoweka kwa tani 1.1 kati ya tani 20 za unga wa mahindi ambao uliwasilishwa katika Kaunti Ndogo ya Nalutuntu kwa wakaazi walioathiriwa na kufungiwa kutotoka nje,” Daily Monitor waliripoti.

"Mwanzoni, washukiwa watatu walisisitiza kuwa chakula kilichotolewa kilikuwa katika mikono salama, lakini tulipohesabu magunia kwenye duka, ilibainika kuwa kilo 1100 za unga wa mahindi hazikuwepo na ndipo walipokamatwa," alisema diwani wa kaunti hiyo ndogo kulingana na Daily Monitor.