Daktari apoteza Ksh 219K za chanjo ya Polio baada ya kupoteza bet kombe la dunia

Pesa hizo zilikuwa zimetumwa kwake ili awalipe wahudumu wa afya waliokuwa wakitoa chanjo ya polio vijijini.

Muhtasari

• Baada ya kuhojiwa, alikubali makosa na kusema angezitafuta ili kuwalipa wahudumu wa afya wenzake.

• Pesa hizo ziliwekwa kwa akaunti yake kuwalipa wahudumu wa afya waliokuwa wakitoa chanjo ya polio vijijini.

Image: Getty Images

Mashindano ya kombe la dunia yakiwa yanaendelea nchini Qatar kwa wiki ya pili sasa, watu mbali mbali wamekuwa wakivuna lakini pia wengine wamekuwa wakiambulia patupu kufuatia kubashiri na kushiriki michezo ya bahati nasibu katika mechi hizo.

Nchini Uganda, dakatari mmoja amejipata pabaya baada ya kutumia pesa za kulipwa wafanyikazi wa afya waliozunguka kote nchini humo kutoa chanjo ya ugonjwa wa polio kwa watoto.

Tukio hilo lililoripotiwa na jarida la New Vision nchini Uganda lilisema kuwa daktari huyo alitumia kima cha milioni 6.7 za Uganda sawa na shilingi elfu 219 za Kenya zilizokuwa zimetengwa kama marupurupu ya kuwalipa wahudumu wa afya, alibashiri nazo mechi za kombe la dunia na mkeka haukufaulu kwani timu aliyoibashiria ilititigwa vibaya mno.

Daktari huyo aliripotiwa kuwa mkaazi wa kata ndogo ya Zombo na ametakiwa kufanya mchakato wa haraka kupata pesa hizo ili wahudumu waliotaabika kutoa chanjo ya polio kote nchini wapate malimbikizi yao.

Kulingana na taarifa hiyo, kamishna wa kata ya Zombo Grace Atim alisema pesa zilitumwa kwa akaunti ya dakatari huyo ili kuwalipa wahudumu wa afya 240, lakini baada ya kuhojiwa kwa kina, alisema alipoteza pesa zote baada ya kuwekeza kwenye mkeka wa kombe la dunia lakini alikubali na kusema angezirudisha baada ya kutafuta usaidizi wa mikopo.

Nchini Qatar, mashindano ya mwaka huu yamekuwa tofauti huku timu kadhaa zikiwashangaza watu kwa kupigwa na kubanduliwa na timu ambazo hazikuwa zimepatiwa upato mkubwa wa kuibuka washindi.

Kwa mfano, wiki jana Morocco iliwashangaza wengi baada ya kuinyuka Ubelgiji ambayo ilikuwa imepewa nafasi kubwa ya kushinda ikizingatiwa kuwa imeshikilia nafasi ya pili katika msimamo wa FIFA huku Morocco wakiwa namba 22.