Tundu Lissu: Nitarejea Tanzania tarehe 25 Januari mwaka 2023

Lissu amesema mwaka huu utakuwa muhimu sana katika historia ya Tanzania.

Muhtasari
  • Amesema hiki kimekuwa kipindi kirefu na kigumu sana katika maisha yake binafsi na kama chama na taifa

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu amesema atarejea Tanzania siku ya Jumatano tarehe 25 mwezi Januari mwaka 2023.

Lissu ameyasema hayo alipokuwa akitoa salamu zake za mwaka 2023 kwa njia ya mtandao akiwa uhamishoni nchini Ubelgiji.

Amesema kuwa hawawezi kuendelea kuishi uhamishoni bila ukomo.

''Nimeishi uhamishoni kwa zaidi ya miaka mitano, kuanzia siku niliyokimbizwa Nairobi Kenya kwa matibabu ya dharura, baada ya jaribio la mauaji dhidi yangu la tarehe 7 Septemba mwaka 2017''

Amesema hiki kimekuwa kipindi kirefu na kigumu sana katika maisha yake binafsi na kama chama na taifa.

''Muda huo ninatarajia kutua uwanja wa ndege wa kimataifa Dsm kwa Ndege ya Shirika la Ndege Ethiopia nikitokea Brussels Ubelgiji....nitafurahi sana kwa mapokezi yoyote mtakayopendezwa kuniandalia siku hiyo''. Alisema Bw. Lissu.

Lissu amesema mwaka huu utakuwa muhimu sana katika historia ya Tanzania.

''Ni mwaka ambao kama tukiamua kwa dhati ya mioyo yetu tutapata katiba mpya na ya kidemokrasia yenye mfumo huru wa uchaguzi inayojali na kulinda haki za wananchi na inayoweka misingi imara ya uwajibikaji wa viongozi wetu kwa wananchi na kwa wawakilishi wao.''

''Rais Samia na Chama chake na serikali wameshaahidi hadharani kwamba wako tayari kuanza safari hiyo ndefu na ngumu.''

‘’Tunawajibika kumjibu Mh.Rais kwa kuonesha na kudhihirisha kwa vitendo kwamba na sisi pia tuko tayari na tumejiandaa kwa safari hiyo kwahiyo ninarudi nyumbani kwa safari hiyo’’. Alisema Bw. Lissu