Mhubiri na polisi watatu washtakiwa kwa madai ya ubakaji Uganda

Polisi wanasema muathiriwa alitapeliwa pesa zake na kunyang'anywa hati yake ya kusafiria.

Muhtasari

•Watatu hao walikamatwa kwa madai ya ubakaji wa mwanamke raia wa Latvia katika nyumba moja katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kampala.

Image: BBC

Mhubiri wa Uganda na maafisa watatu wa polisi wamekamatwa kwa madai ya ubakaji wa mwanamke raia wa Latvia katika nyumba moja katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kampala.

Polisi wanasema muathiriwa alitapeliwa pesa zake na kunyang'anywa hati yake ya kusafiria.

Haijafahamika bado iwapo washukiwa wametoa maoni yao kuhusu mashtaka hayo.

Mhubiri huyo alikuwa amemwalika mwanamke huyo kuzuru nchini Uganda na aliwasili takriban mwezi mmoja uliopita, taarifa ya polisi ilisema.

Maafisa watatu walioshughulikia kesi hiyo wakati muathiriwa alipowasilisha malalamiko yake katika kituo cha polisi cha Jinja Road wanakabiliwa na mashtaka ya utovu wa nidhamu.

Muathiriwa anawashutumu kwa kumfungia mbaroni na kumlazimisha kuweka sahihi katika taarifa ya kukiri kupokea malipo ya pesa zake zote na kufutwa kwa kesi dhidi ya mhubiri.

Idara ya polisi ya Upelelezi wa Jinai sasa imechukua kesi hiyo na kumtaka yeyote aliye na malalamiko dhidi ya mhubiri huyo kuripoti kwao.