Vita vya Ukraine: Kamanda wa Wagner Group ya Urusi aiomba Norway hifadhi

Andrey Medvedev, 26, alivuka mpaka na kuingia Norway Ijumaa iliyopita.

Muhtasari

• Anazuiliwa katika eneo la Oslo akikabiliwa na mashtaka ya kuingia Norway kinyume cha sheria.

Kamanda wa zamani wa kundi la wapiganaji la Urusi Wagner ameomba hifadhi nchini Norway baada ya kutoroka kutoka kundi hilo la mamluki.

Andrey Medvedev, 26, alivuka mpaka na kuingia Norway Ijumaa iliyopita, ambapo alizuiliwa na walinzi wa mpaka.

Kwa sasa anazuiliwa katika eneo la Oslo ambako anakabiliwa na mashtaka ya kuingia nchini Norway kinyume cha sheria, wakili wake Brynjulf​​Risnes aliambia BBC.

Bw Risnes alisema mteja wake aliondoka Wagner baada ya kushuhudia uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

Kikosi cha Walinzi wa Mipaka cha Norway kiliithibitishia BBC kwamba mwanamume wa Urusi alizuiliwa baada ya kuvuka mpaka wa nchi hiyo wenye urefu wa kilomita 198 (maili 123) na Urusi, lakini ilisema haiwezi kutoa maoni zaidi kwa "sababu za usalama na faragha".

Tarjei Sirma-Tellefsen, mkuu wa polisi katika eneo la Finnmark nchini Norway, alisema mwanamume mmoja amezuiliwa na walinzi wa mpakani na kusema kuwa ameomba hifadhi.

Lakini kundi la kutetea haki za binadamu la Urusi ,Gulagu, ambalo lilimsaidia Bw Medvedev kuondoka Urusi, lilithibitisha utambulisho wake. Kutoroka kwake kunaaminika kuwa tukio la kwanza linalojulikana la mmoja wa wanajeshi wa kundi hilo kuhamia nchi za Magharibi.

Mwanzilishi wa Gulagu Vladimir Osechkin aliambia BBC kwamba Bw Medvedev alijiunga na kundi la wanamgambo mnamo Julai 2022 kwa kandarasi ya miezi minne, lakini alitoroka baada ya kushuhudia ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita alipokuwa akihudumu nchini Ukraine.

Alisema kuwa Bw Medvedev ni mwanajeshi wa zamani katika jeshi la Urusi na kwamba baadaye alitumikia kifungo kati ya 2017 na 2018 kabla ya kujiunga na Kundi la Wagner.