Familia yathibitisha kifo cha raia wa Tanzania vitani nchini Ukraine

Kwa mujibu wa familia, Tarimo alifariki mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Muhtasari

• Taarifa ya kwanza walipatiwa na marafiki wa karibu mwishoni mwa mwezi Desemba kuwa kijana wao amefariki.

• Baadaye familia ilipata taarifa rasmi kutoka Ubalozi wa Tanzania huko Moscow.

Image: NEMES/FACEBOOK

Taarifa za kifo cha Raia wa Tanzania, Nemes Tarimo, zilisambaa pamoja na video ikionesha  akiwa anaagwa kwa heshima na vikosi vya jeshi nchini Urusi.

Familia ya Nemes Tarimo imethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuwa wanasubiri mwili wa mpendwa wao kwa ajili ya Maziko.

Kwa mujibu wa familia, Tarimo alifariki mwishoni mwa mwezi Oktoba na kwamba taarifa ya kwanza walipatiwa na marafiki wa karibu mwishoni mwa mwezi Desemba kuwa kijana wao amefariki. Baadaye walipata taarifa rasmi kutoka Ubalozi wa Tanzania huko Moscow.

BBC imejaribu kutafuta mamlaka za Tanzania bila mafanikio.

Hatukuamini kama amekufa

Baada ya kupokea taarifa za kifo chake, ilikua ngumu kwa familia kuamini taarifa hizo, lakini baada ya video ya kuagwa kwakwe kusambaa ndio walianza kuona kuwa kweli kijana wao amefariki.

‘’Kwakweli hatukuamini kabisa, lakini baadae video ikaanza kusambaa na kuangalia majina yake yote matatu ni sahihi ndio tukajua kweli kijanza wetu ametutoka, lakini bado hatuamini hadi tuone mwili wake’’ anasema mama mlezi wa Nemes.

Mwili wa Tarimo ilikua urudishwe wiki kadhaa zilizopita lakini hadi sasa bado familia haijapokea mwili huo.

Image: NEMES/FACEBOOK

Ilkuaje hadi akafariki nchini Ukraine?

Kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa Tarimo, alikamatwa kwa kesi ya dawa za kulevya kisha akafungwa, baada ya muda alipatiwa taarifa za kujiunga na kundi la Wagner na kuahidiwa kuachiwa huru baada ya miezi sita ya kupambana katika uwanja wa vita.

‘’Alitupatia taarifa kuwa anajiunga kwenda kwenye vita dhidi ya Ukraine, tulimsihi sana asijiunge lakini akasema huwezi jua nitapata uhuru wangu kwa hiyo akajiunga na mara ya mwisho kuwasiliana ilikua Oktoba 17 na hakupatikana tena, ’’anasema ndugu wa Nemes ambaye hakutaka jina lake  

Nemes alienda Urusi kwa ajili ya masomo ya shahada ya uzamili katika Chuo cha Teknolojia cha Urusi, MIREA.

Nemes Tarimo 33, anatajwa kama kijana mpole na mchagamfu sana na mtu wa dini. Wazazi wake walifariki mapema na kusababisha Nemes kulelewa na ndugu upande wa mama yake.

‘’Alikua kijana mpole sana, lakini mchangamfu na kwakweli alikuwa na msaada mkubwa kwa familia, pia alikuwa mtu wa dini sana na akipenda masomo na kujiendeleza’’ anasema mmoja wa ndugu zake.

Alisoma shule ya Sekondari Tosa Maganga iliyopo nyanda za juu Kusini mwa Tanzania kisha akajiunga na masomo ya chuo kikuu akisomea shahada ya Teknolojia. Alifanya kazi katika mashirika mbalimbali kabla ya kupata fursa ya kujiendeleza kimasomo nchini Urusi.

Raia wa Zambia, Lemekhani Nyirenda, 23, alifariki nchini Ukraine akiipigania Urusi, naye awali alikuwa akitumikia kifungo kinachohusiana na dawa za kulevya nchini Urusi lakini aliachiliwa na kupelekwa mstari wa mbele nchini Ukraine.

Alifariki tangu mwezi Septemba, mwaka jana lakini familia yake ilichelewa kupata taarifa na mwili wake ulirudishwa nchini Zambia mwezi Desemba.

Wagner ni kundi gani?

Kundi la Wagner kwa mara ya kwanza liliibuka mashariki mwa Ukraine mwaka wa 2014 ambapo liliwasaidia watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi kupata udhibiti wa eneo la Ukraine na kuanzisha jamhuri mbili zilizojitenga katika mikoa ya Donetsk na Luhansk.

Tangu 2014, kundi la Wagner limeshiriki katika migogoro kadhaa duniani kote, hasa nchini Syria na katika nchi nyingi za Afrika.

 Mmiliki wa kundi hilo Yevgeny Prigozhin ambaye pia ni mshirika wa karibu wa rais wa Urusi Vladmiri Putin,  Mnamo Septemba mwaka jana, miezi sita baada ya uvamizi wa Urusi wa Ukraine, ghafla alikiri kwamba alikuwa ameanzisha kundi la Wagner kama lilioonekana kuwa moja ya vitengo vya ufanisi zaidi vya Kirusi katika vita.