Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak apigwa faini kwa kutofunga mkanda ndani ya gari

Sunak alikubali kabisa kuwa hili lilikuwa kosa na akaomba msamaha, na kuongeza kuwa atalipa faini hiyo.

Muhtasari

• Nchini Uingereza, notisi za adhabu zisizobadilika ni adhabu ya kukiuka sheria, na inamaanisha faini, ambayo inahitaji kulipwa ndani ya siku 28, au kupingwa.

Waziri mkuu wa UK, Rishi Sunak
Waziri mkuu wa UK, Rishi Sunak
Image: BBC

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak amepigwa faini kwa kutofunga mkanda wa kiti kwenye gari lililokuwa linatembea wakati akirekodi video kwenye mitandao ya kijamii.

Kulingana na majarida ya Uingereza, Polisi wa Lancashire walisema kuwa wamempa waziri huyo mkuu wa miaka 42 kutoka London na faini ya masharti ya adhabu isiyobadilika.

Nambari 10 alisema Bw Sunak "anakubali kabisa kuwa hili lilikuwa kosa na ameomba msamaha", na kuongeza kuwa atalipa faini hiyo.

Abiria wanaopatikana wakiwa hawajafunga mikanda ya usalama nchini Uingereza huwa wanatozwa faini ya £100 ambazo ni sawa na shilingi elfu 15 pesa za Kenya.

Video hiyo ambazo ilimletea matatizo ilipakiwa kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo Sunak alikuwa anaonesha hatua za hivi punde ambazo serikal iyake imepiga, miezi michache tu tangu alipoapishwa kama waziri mkuu kufuatia kujiuzulu kwa Liz Truss.

Ni mara ya pili kwa Bw Sunak kupokea notisi ya adhabu isiyobadilika akiwa serikalini.

Aprili mwaka jana, alitozwa faini pamoja na Boris Johnson na mkewe Carrie kwa kuvunja sheria za kufunga Covid - kwa kuhudhuria mkusanyiko wa siku ya kuzaliwa kwa waziri mkuu wa wakati huo huko Downing Street mnamo Juni 2020.

Faini hiyo inaweza kuongezeka hadi £500 ikiwa kesi itaenda mahakamani.

Nchini Uingereza, notisi za adhabu zisizobadilika ni adhabu ya kukiuka sheria, na inamaanisha faini, ambayo inahitaji kulipwa ndani ya siku 28, au kupingwa.

Iwapo mtu atachagua kupinga faini hiyo, basi polisi watapitia kesi hiyo na kuamua kama wataiondoa faini hiyo au kupeleka suala hilo mahakamani.