Kutokana na ubakaji wa Tyson, niliteseka na kuumia kimwili, kisaikolojia na kihisia - Mwathiriwa asimulia

Mwathiriwa huyo alisema bondia Mike Tyson alimfuata kwa gari lake la Limousine na kumtendea unyama huo mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Muhtasari

• Hii si mara ya kwanza kwa Tyson kukabiliwa na kesi ya ubakaji.

• Mwaka wa 1992 alipatikana na hatia ya kumbaka mwanamitindo Desiree Washington na kufungwa jela kwa miaka 3.

Bondia wa zamani wa Marekani Mike Tyson
Bondia wa zamani wa Marekani Mike Tyson
Image: screenshot//YouTube

Mwanabondia nguli wa miaka ya 90 Mike Tyson anaendelea kuandamwa na matatizo ya kila aina kufuatia vitendo ambavyo alivitekeleza kwa kutumia ushawishi wa umaarufu wake nje ya ulingo wa ndondi miaka hiyo akiwa amenawiri katika mchezo huo.

Hii ni baada ya Mwanamke mmoja katika jimbo la New York kufungua kesi ya madai dhidi ya Mike Tyson, akimshutumu bingwa huyo wa zamani wa ndondi kwa kumbaka akiwa kwenye gari la Limousine mwanzoni mwa miaka ya 1990, kulingana na kesi mahakamani.

Mwanamke huyo, ambaye aliomba mahakama isitaje jina lake, aliwasilisha malalamiko yake mapema Januari chini ya sheria ya muda ya jimbo la New York inayoruhusu waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia kutafuta fidia ya kiraia bila kujali sheria ya vikwazo.

Itakumbukwa hii si mara ya kwanza kwa mwanamasumbwi huyo kukabiliwa na kesi za sampuli hiyo kwani aliwahi kaa jela miaka mitatu kuanzia 1992 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanamitindo Desiree Washington, ambaye alikuwa na umri wa miaka 18 wakati huo.

Kulingana na jarida la AFP, hati fupi ya kiapo ya Desemba 23, 2022 ilitolewa ambapo mlalamikaji anasema kwamba alikutana na bondia huyo kwenye kilabu cha usiku "mapema miaka ya 1990," kisha akamfuata ndani ya gari lake la Limousine, ambapo alidaiwa kumvamia kabla ya kumbaka.

"Kutokana na ubakaji wa Tyson, niliteseka na ninaendelea kuumia kimwili, kisaikolojia na kihisia," alisema.

Anatafuta fidia ya dola milioni 5.

Kufikia Jumanne jioni, Tyson alikuwa hajatoa taarifa yoyote kwa umma, AFP walisema.

Mzaliwa huyo wa Brooklyn mwaka wa 1966, Tyson alipata matatizo ya utotoni kabla ya kuwa bingwa asiyepingika wa uzito wa juu katika miaka ya 1980, akiwatisha wapinzani wake kwa hasira yake katika ulingo na ngumi za ajabu.

Lakini baada ya kifungo chake gerezani, hakuweza kuhifadhi vyeo vyake.