Vikosi vya Marekani vyamuua kiongozi mkuu wa Islamic State nchini Somalia

Al-Sudani, amekuwa chini ya uangalizi wa maafisa wa kijasusi wa Marekani kwa miaka mingi,

Muhtasari

• Bilal Al-Sudani anadaiwa kuwa mhusika mkuu katika ufadhili na upanuzi wa kundi la wanamgambo wa Kiislamu barani Afrika na kwingineko.

Image: BBC

Marekani inasema kuwa vikosi vyake maalum vimemuua kiongozi mkuu wa kundi la Islamic State nchini Somalia, pamoja na washirika wake 10.

Bilal Al-Sudani anadaiwa kuwa mhusika mkuu katika ufadhili na upanuzi wa kundi la wanamgambo wa Kiislamu barani Afrika na kwingineko.

Maafisa wanasema aliuawa wakati wa mapigano ya risasi baada ya wanajeshi kuvamia eneo la pango la milimani kaskazini mwa Somalia, wakitarajia kumkamata. Katika taarifa yake Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alisema hakuna raia aliyejeruhiwa katika kile alichokitaja kuwa "operesheni yenye mafanikio ya kukabiliana na ugaidi."

Je, ISIS inaweza kuathirika vipi na mauaji ya Bilal Al-Sudani?

"Bilal alikuwa mwanachama muhimu. Kifo chake kinaleta athari kwa kundi hilo kwa sababu ndiye aliyekuwa msimamizi wa fedha za Daesh nchini Somalia na Afrika kwa ujumla. Alipouawa kundi hilo litadhoofika sana." Kanali Abhid Mohamud Hassan aliambia BBC

Al-Sudani, ambaye amekuwa chini ya uangalizi wa maafisa wa kijasusi wa Marekani kwa miaka mingi, amekuwa na jukumu muhimu katika kufadhili operesheni za IS barani Afrika pamoja na operesheni zinazofanana na ISIS nchini Afghanistan, Austin alisema. Idara ya Hazina ya Marekani mwaka jana ilishutumu Al-Sudani kwa kufanya kazi kwa karibu na afisa mwingine wa IS, Abdullah Hussein Abadigga, ambaye aliajiri vijana kutoka Afrika Kusini na kuwapeleka kwenye kambi ya mafunzo.