Rasmi! Trump kurejeshewa akaunti zake za Facebook na Instagram

Facebook ilimpiga marufuku Trump siku moja baada ya vuguvugu la Januari 6, 2021 wafuasi wake wakijitoma ndani ya Capitol kwa fujo.

Muhtasari

• Mwezi Novemba mwaka jana, Twitter walimrejeshea Trump akaunti yake iliyofungwa pia kufuatia vurugu za uchaguzi uliopita.

Facebook kutathmni kurudisha Trump
Facebook kutathmni kurudisha Trump
Image: Maktaba, Wikipedia

Kampuni kubwa ya mtandao wa kijamii ya Meta ilitangaza Jumanne kwamba hivi karibuni itarejesha akaunti za rais wa zamani wa Markani Donald Trump kwenye Facebook na Instagram.

Kampuni hiyo ilisema kuwa itampa Trump masharti mapya na miongozo ya kufuata, miaka miwili baada ya kupigwa marufuku kwa sababu ya uasi wa 2021 wa ikulu ya Marekani, Capitol.

"Tutarejesha akaunti za Bw. Trump za Facebook na Instagram katika wiki zijazo," Nick Clegg, rais wa masuala ya kimataifa wa Meta, alisema katika taarifa yake kama ilivyonukuliwa na AFP, akiongeza kwamba hatua hiyo itakuja na "ulinzi mpya ili kuzuia makosa yanayorudiwa."

Kuendelea mbele, kiongozi wa Republican -- ambaye tayari amejitangaza kuwa mgombea urais wa 2024 -- anaweza kusimamishwa kwa hadi miaka miwili kwa kila ukiukaji wa sera za jukwaa, Clegg alisema.

Haikuwa wazi ni lini au ikiwa Trump atarejea kwenye majukwaa, na wawakilishi wake hawakujibu mara moja ombi la maoni.

Lakini tajiri huyo mwenye umri wa miaka 76 alijibu kwa mtindo wa kawaida, akisema kwamba Facebook ilikuwa imepoteza "thamani ya mabilioni ya dola" bila kuwepo kwake.

"Jambo kama hilo halipaswi kutokea tena kwa Rais aliye madarakani, au mtu mwingine yeyote ambaye hastahili kuadhibiwa!" alisema kwenye jukwaa lake la Truth Social.

Facebook ilimpiga marufuku Trump siku moja baada ya vuguvugu la Januari 6, 2021, wakati kundi la wafuasi wake waliotaka kusitisha uidhinishaji wa kushindwa kwake katika uchaguzi na Joe Biden walipovamia Ikulu ya Marekani mjini Washington.