Rais Suluhu aomba kukutana na mrembo aliyemtakia heri njema ya kuzaliwa Twitter

Mwanadada huyo aliandika ujumbe wa kawaida tu bila kutarajia kujibiwa na rais Hassan, lakini kwa mshangao rais akajibu kutaka kukutana naye.

Muhtasari

• Mwanadada huyo alimtakia kheri njema ya kuzaliwa ambapo pia siku hiyo naye alikuwa anasherehekea kuzaliwa kwake.

• Alisema ombi lake siku moja ni kukutana na rais Suluhu ili kuzungumzia suala la afya ya kina mama.

Rais Suluhu Hassan kukutana na mwandada aliyemwandiia ujumbe Twitter
Rais Suluhu Hassan kukutana na mwandada aliyemwandiia ujumbe Twitter
Image: Twitter

Ijumaa ya Januari 27 rais wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan alikuwa anasherehekea siku yake ya kuzaliwa. Watu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii walifurika kumsherehekea na kumpa pongezi kwa kuona mwaka mwingine.

Mwanadada mmoja kwa jina Vivian Joseph, ambaye pia alikuwa anasherehekea siku yake ya kuzaliwa sambamba na rais aliamua kuelekea mtandao wa Twitter na kupakia picha yake akijisherehekea huku pia akimsherehekea rais Suluhu kwa ujumbe huo mmoja.

Asichokuwa anakijua ni kwamba rais Suluhu Hassan zaidi ya saa 10 baadae angefurahishwa na ujumbe wake na kuujibu huku akisema kuwa angependa kukutana na mwanadada huyo.

Wengi wanaweza sema kuwa mwanadada huyo aliandika ujumbe wenye makopakopa mengi na lugha changamano. La hasha! Ujumbe wake ulikuwa wa kawaida tu lakini nyota ya rais ikauangazia.

“Ninasherehekea siku yangu ya kuzaliwa na Mheshimiwa Mama Rais Samia Suluhu. Nina nia moja kwa mwaka huu siku moja kuwa na mazungumzo naye kuhusu masuala ya afya katika Kanda ya SADC. Nitanyenyekea sana. Happy birthday Madam President,” mwandada huyo alitweet.

Saa kumi na moja baadae, rais Suluhu kuingia kwenye Twitter huo ndio ujumbe aliuona wa kwanza miongoni mwa maelfu ya jumbe zilizokuwa zikimtakia kheri njema ya siku ya kuzaliwa.

Naye rais hakuwa mchoyo wa fadhila, ali’retweet ujumbe wa mwanadada yule na kumtakia khri njema ya kuzaliwa pia huku akifichua kuwa tayari alishafanya mawasiliano na wasaidizi wake ili kufanikisha ndoto ya mwanadada huyo kutaka kukutana naye katika ikulu.

“Heri ya Siku ya Kuzaliwa Vivian, na asante kwa matakwa. Wasaidizi wangu watakufikia ili kupanga mkutano. Natarajia kuzungumza na wewe,” mama Samia Suluhu Hassan alimjibu kwa upole na uzuri wa aina yake.

Kwa asilimia kubwa, tunaweza sema Mwanadada huyo bila shaka hakuwa na matumaini hata chembe kuwa rais angejibu ujumbe. Lakini nyota ya Mungu ikiamua kutua kwenye panda la uso wake, hakuna atakayeizima.

Sasa Vivian Joseph anatarajiwa kuwa na kikao cha moja kwa moja na rais Samia huku wakizungumzia masuala tete ya afya ya kina mama!