Mzee aliyepotea akiwa na miaka 45 arejea nyumbani akiwa na miaka 111

Mzee huyo alitoroka nyumbani mwaka 1957 baada ya kupoteza mchezo wa kamari uliotishia mali yake kupigwa tanji.

Muhtasari

• Kipindi anaondoka, hakuna taifa hata moja katika ukanda wa Afrika Mashariki lilikuwa limejinyakulia uhuru.

• Watu wa ukoo wake walimtafuta wakapoteza matumaini kwani kipindi hicho hakukuwa na mawasiliano kwa njia ya simu.

Mzee Patrick Okubal
Mzee Patrick Okubal
Image: Screengrab//Youtube,

Ilikuwa ni hali ya furaha na mshangao kwa wakati mmoja baada ya Mwanamume mmoja kutoka wilaya ya Sorot nchini Uganda kurejea nyumbani baada ya kutoweka kwa miaka 66.

Kulingana na taarifa kutoka vyombo vya taifa hilo jirani, Patrick Okubal alitoweka nyumbani mwaka 1957 akiwa na umri wa miaka 45 tu na juhudi za familia yake kumfikia ziligonga mwamba kwani kipindi hicho hakukuwa na simu za rununu na mataifa ya Afrika Mashariki hayakuwa yamejinyakuliwa uhuru kutoka kwa mkoloni.

Okubal ambaye sasa ana umri wa miaka 111 alirejea kijijini kwa mababu zake akiwa na watu wa ukoo wake kutoka Wilaya ya Bukwo na kupokelewa kwa furaha na sherehe ya siku mbili iliyoshuhudia familia hiyo ikichinja ng'ombe, mbuzi na kufanya maombi ya shukrani.

“Akiwa amezaa watoto watano wakati wa kutoweka kwake, Okubal alikaribishwa na watoto wake wawili pekee waliosalia, Pascal Awojat, 66 na Bi Rupina Amongin, 70, pamoja na wajukuu 139,” taarifa ilisema.

Okubal anaaminika kuondoka nyumbani kwake baada ya kuripotiwa kupoteza utajiri wake kwa mchezo wa kamari, unaojulikana miongoni mwa Waiteso kama Epiki ambapo alihatarisha utajiri wa familia yake hatua kwa hatua hadi kumjumuisha mkewe.

Familia hiyo ilieleza furaha na shukrani kwa familia ya Bukwo kwa kumweka baba yao salama kwa takriban miongo saba na kumaliza msako wao wa kukata tamaa, ambao hata hivyo walikiri kuwa tayari wameuacha zaidi ya miaka 10 iliyopita.

"Tulijaribu lakini njiani, tulizuia utafutaji wowote. Kilicho muhimu ni kujiokoa kwetu sisi wenyewe,” binti wa Okubal ambaye alishindwa kuficha furaha yake alisema.

Katika maisha yake yote uhamishoni, Okubal alisemekana kuwa hakuwa na uhusiano wowote wala hakuwa na watoto wengine.