Nilimaanisha ushoga si uhalifu, lakini ni dhambi - Pope Francis anyoosha maelezo

"Kwanza tutofautishe kati ya dhambi na uhalifu,” - Pope Francis alisema.

Muhtasari

• Papa aliongeza zaidi kwamba alimaanisha kusema kwamba kuharamishwa kwa ushoga “si jambo zuri wala la haki.”

Pope Francis
Pope Francis
Image: Hisani

Papa Francis wa kanisa Katoliki sasa amejitokeza wazi kutetea matamshi yake kuhusu wanachama wa LGBTQ ambayo yaligonga vichwa vya habari wiki jana.

Katika barua aliyomwandikia Padre Mjesuiti James Martin ambaye alimfikia Papa kupata ufafanuzi zaidi kuhusu tamko hilo ambalo lilionekana kuzua nyufa kubwa miongoni mwa waumini wa Kikatoliki kote duniani, Francis alifafanua kuwa kuna tofauti kubwa kuhusu ushoga, uhalifu na dhambi.

Francis alisema “Niliposema ni dhambi, nilikuwa nikimaanisha tu mafundisho ya maadili ya Kikatoliki, ambayo yanasema kila tendo la ndoa nje ya ndoa ni dhambi.”

Papa aliongeza zaidi kwamba alimaanisha kusema kwamba kuharamishwa kwa ushoga “si jambo zuri wala la haki.”

"Kama unavyoona, nilikuwa narudia kitu kwa ujumla. Nilipaswa kusema ‘Ni dhambi, kama ilivyo tendo lolote la ngono nje ya ndoa.’ Hii ni kuzungumzia ‘suala’ la dhambi, lakini tunajua vyema kwamba maadili ya Kikatoliki hayatilii maanani suala hilo tu bali pia yanatathmini uhuru. na nia; na hii, kwa kila aina ya dhambi.”

Wakati wa mahojiano na AP siku ya Jumanne wiki jana, Francis alibaini kuwa kufanya mapenzi ya jinsia moja sio kosa, kauli ambayo ilikumbatiwa na kusambazwa pakubwa na vyombo vya habari huku waumini wa Kikatoliki na Wakristu kwa ujumla kote duniani wakiwa na maoni kinzani.

“Kulawiti si kosa. Sio uhalifu. Ndio, lakini ni dhambi. Sawa, lakini kwanza tutofautishe kati ya dhambi na uhalifu,” aliiambia AP.

Alizitaja sheria zinazoharamisha mapenzi ya jinsia moja kuwa ni “zisizo za haki” na kwamba lazima Kanisa lifanye kazi ili kuzikomesha.