Mfanyibiashara wa kiume wa miaka 25 afariki ndani ya loji akiwa na mpenziwe

Mwathiriwa anaripotiwa kuanguka ghalfa na kuzimia akiwa chumbani na kidosho huyo.

Muhtasari

• Musstafa alifariki Januari 25 mwendo wa saa tisa alasiri kutokana na kushindwa kupumua.

Crime Scene
Image: HISANI

Polisi nchini Uganda katika kanda ya Magharibi mwa Mto Nile wanachunguza kisa ambapo mwanamume mmoja aliyetajwa kama mfanyibiashara kufariki ndani ya chumba cha kulala wageni saa chache baada ya kuingia hapo na mpenzi wake wa kike.

Marehemu aliyetambuliwa kwa jina Ali Musstafa ni mfanyibiashara maarufu katika wadi ya Kenya wilayani Arua nchini humo na anadaiwa kufariki akiwa anavunja amri ya saba na mpenzi wake ndani ya gesti.

“Mwathiriwa alianguka na kufia chumbani. Msichana huyo alienda na kuwajulisha wasimamizi wa hoteli ambao mara moja walitoa taarifa kwa polisi wa Arua. Tukio hilo lilitembelewa na kurekodiwa vizuri, hakuna chembe ya dawa, sumu au athari zingine za mwili zilizopatikana kwenye eneo la tukio. Mwili ulihamishwa hadi Hospitali ya Rufaa ya Arua na kufanyiwa uchunguzi,” msemaji wa Polisi, SCP Fred Enanga alinukuliwa na jarida la Monitor nchini humo.

Kulingana naye, Musstafa alifariki Januari 25 mwendo wa saa tisa alasiri kutokana na kushindwa kupumua kabla ya mwili wake kuchukuliwa kutoka chumba cha hoteli na kufanyiwa uchunguzi wa maiti.

"Kifo wakati wa kujamiiana kwa maelewano kinaweza kutokea kwa sababu kadhaa, ambazo ni pamoja na mkazo wa kimwili wa shughuli au kwa sababu ya hali zisizo za kawaida," SCP Enanga aliongeza.

Tukio hili linakuja wiki moja baada ya tukio sawia kuripotiwa jijini Nairobi baada ya mwanamume mzee wa miaka 71 kufariki kwenye gesti akiwa na kidosho wa miaka 22.

Inaarifiwa kuwa kidosho huyo aliwataarifu watu wa gesti hilo baada ya mzee huyo kupata matatizo ya kupumua, gari liliitwa kumpeleka katika hospitali ya Agha Khan lakini alifariki kwa bahati mbaya.