Ethiopia yafukuza vyombo vya habari vya kigeni kwa kufichua ufisadi na ukame mkali

Taarifa zilisema kwamba takribani vyombo vya habari vya kigeni vipatao 15 viliathirika na marufuku hiyo.

Muhtasari

• Tangu kuzuka kwa mgogoro wa Tigray Kaskazini mwa Ethiopia, uhuru wa vyombo vya habari nchini humo umekuwa ukikabiliwa na changamoto si haba.

Wanahabari kazini
Wanahabari kazini
Image: MAKTABA

Mamlaka ya Ethiopia imesimamisha vyombo vya habari 15 vya kigeni ambavyo vimekuwa vikifanya kazi katika jimbo la kanda ya Somalia kwa madai ya kufanya kazi bila leseni.

Chama cha wanahabari wa kanda hata hivyo kinasema hatua hizo zilichukuliwa kulipiza kisasi ripoti za vyombo vya habari zilizofichua ufisadi na ukame mkali unaoikabili kanda hiyo.

Kusimamishwa huko kunakuja siku chache baada ya chombo kikuu cha udhibiti wa vyombo vya habari cha serikali ya shirikisho, Mamlaka ya Vyombo vya Habari vya Ethiopia (EMA) kupitisha agizo la kuagiza mamlaka za kikanda kupiga marufuku vyombo vya habari, majarida yanaripoti.

Katika barua iliyoandikwa tarehe 27 Januari, Mamlaka ya Vyombo vya Habari ya Ethiopia (EMA) ilihimiza Ofisi ya Mawasiliano ya Kanda ya Somalia kuchukua hatua kwa ushirikiano na vyombo vya sheria kwa watu binafsi wanaofanya kazi kwa vyombo vya habari vya kigeni bila kuwa na leseni za vyombo vya habari.

Barua hiyo ilisema mamlaka hiyo imegundua katika uchunguzi kuwa kuna wawakilishi wa vyombo vya habari na waandishi wa habari ambao wanafanya kazi katika jimbo hilo bila ya kuwa na leseni kutoka kwa chombo cha udhibiti wa vyombo vya habari vya serikali ya shirikisho.

Hata hivyo barua hiyo haikuweka wazi majina ya vyombo hivyo vinavyodaiwa kuwa ni vyombo vya habari.

Mafuruku hii inakuja wakati ambapo kumekuwa na tuhuma kwamba baadhi ya viongozi wa serikali hawataki hali mbaya ya ukame kuonekana na jamii za kimataifa ili kutoa msaada kwa hofu kuwa watachafua picha yao machoni mwa jamii ya kimataifa.

Aidha, Tangu mzozo katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia ulipozuka Novemba 2020, uhuru wa vyombo vya habari nchini Ethiopia umezorota kwa kiasi kikubwa.