Ajali yaua 17 Tanzania ikihusisha gari iliyobeba maiti kwenda kuzikwa

Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na uzembe wa dereva.

Muhtasari

•Watu wengine 12 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia Jumamosi mkoani Tanga Kaskazini mwa Tanzania.

• Ajali hiyo imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso na Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na abiria 26 ikitokea Dar es Salaam kwenda Moshi kwenye mazishi.

Image: BBC

Watu 17 wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi mkoani Tanga Kaskazini mwa Tanzania.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba ilisema ajali hiyo imetokea usiku katika barabara ya Segera - Buiko iliyopo wilayani Korogwe, katika mkoa huo.

Taarifa hiyo imeelezwa kuwa ajali hiyo imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso na Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na abiria 26 ikitokea Dar es Salaam kwenda Moshi kwenye mazishi.

"Ajali hii imesababisha vifo 17 na majeruhi 12 ambao majina yao wote hayajafahamika, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Korogwe na majeruhi 10 wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo na majeruhi wawili wamebaki Hospitali ya Korogwe kwa matibabu," alisema Mkuu huyo wa Mkoa na kuongeza kuwa bado miili haijatambuliwa.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa,chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na uzembe wa dereva lori la kulipita gari la mbele bila ya kuchukua tahadhari na kugongana na basi la abiria.