Mfahamu Waziri mkuu mpya wa China

Mawaziri wapya wanatarajiwa kutangazwa Jumapili.

Muhtasari
  • Kiongozi huyo mpya mwenye umri wa miaka 63 alipigiwa karibu kura zote kutoka kwa wajumbe 2900 katika bunge la nchi.
Image: KWA HISANI

Li Qiang, aliyekuwa kiongozi wa chama cha kikomyunisti katika mji mkubwa nchini humo Shanghai, sasa ataiongoza serikali akiwa anaichukuwa nafasi ya Waziri mkuu aliyekuweko na anayestaafu Li Keqiang.

Kiongozi huyo mpya mwenye umri wa miaka 63 alipigiwa karibu kura zote kutoka kwa wajumbe 2900 katika bunge la nchi.

Mshirika wa karibu wa rais Xi, Qiang anaonekana kama mtu mwenye busara na mchapa kazi na atakuwa na jukumu la kufufua uchumi wa China unaojikokota.

Mawaziri wapya wanatarajiwa kutangazwa Jumapili.

Waandishi habari hawakuruhusiwa ukumbini wakati kura zikipigwa katika mkutano wa kumuidhinisha bungeni.

Makofi yalipigwa wakati rais Xi alipotumbukiza kura yake.

Li – ambaye sasa ni kiongozi wa pili mkubwa kimadaraka katika mfumo wa siasa China, alipokea takriban kura 2,936 huku wajumbe watatu pekee wapiga kura kutoidhinisha uteuzi wake na wanane wakiamua kususia kura hiyo.

Alikula kiapo baada ya hapo, akiahidi kuwa mtiifu kwa katiba ya China na "kuwajibika kujenga nchi yenye ustawi, thabiti demokrasia na ujamaa wa kileo".

Li alikuwa mkuu wa utumishi wa umma chini ya urais wa Xi mapema mwaka 2000 wakati rais Xi alikuwa mkuu wa chama katika jimbo la Zhejiang.

Li aliteuliwa kuwa katibu wa chama katika mji wa Shanghai mnamo 2017.

Wakati wa janga la Covid, alisimamia amri kali ya kutotoka nje mjini Shanghai, jambo lililopelekea baadhi ya wakaazi kukabiliwa na changamoto kupata chakula na huduma za afya.

Uteuzi wake unafanyika baada ya rais Xi kujishindia muhula wa tatu uongozini Ijumaa.

Rais ameukita utawala wake wakati China inaanza kufunguka baada ya sera za kutokomoeza maambukizi ya Covid 19 iliochangia maandamano dhidi ya serikali.

Taifa hilo pia linakabiliwa na kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa jambo linalotishia mpango wa kuukuza uchumi wa nchi.

Vikao vya bunge na vya ushauri wa kisiasa (CPPCC) baadaye wiki hii vinatazamwa kwa karibu wakati vikitarajiwa kutoa muelekeo wa taifa hilo katika miaka ijayo.

Tangu utawala wa Mao Zedong, viongozi wa China wamehudumu kwa mihula miwili.

Wakati rais Xi alipobadili sheria hiyo mnamo 2018, kilimbadili kuwa kiongozi mwenye ushawishi ambao haujawahi kushuhudiwa tangu mwenyekiti Mao.