Waendesha baiskeli waandamana uchi barabarani wakiteta ajali nyingi dhidi yao

Mamia ya waendesha boda boda hao, wake kwa waume walijitosa barabarani na baiskeli zao wakiwa uchi wa mnyama.

Muhtasari

• Video za mitandaoni zinawaonesha wakiendesha baiskeli barabarani uchi wa hayawani wakilalamikia ukatili wa watumizi wa magari kuwasababishia ajali.

Waendesha baiskeli wakiandamana kulalamikia ajali.
Waendesha baiskeli wakiandamana kulalamikia ajali.
Image: Bloomberg,

Wikendi iliyopita, tukio lisilo la kawaida lilishuhudiwa katika jiji la Brazil, Sao Paulo baada ya mamia ya watumizi wa barabara kwa kutumia baiskeli kujitosa kwa maandamano.

Cha kushangaza ni kwamba waendesha baiskeli hao ambao walikuwa na baiskeli zao katika maandamano hayo walikuwa uchi wa mnyama, huku wakilalamikia kukithiri kwa visa vya ajali za makusudi dhidi yao, ajali ambazo walisema zinasababishwa na watumizi wengine wa barabara kwa kutumia magari.

“Waendeshaji wengi kwenye Barabara ya Paulista, mojawapo ya mtaa wenye shughuli nyingi zaidi katika mji mkuu wa kiuchumi wa Brazili, kwa kweli walikuwa uchi. Baadhi, kwa kiasi zaidi, walipendelea kuvaa chupi ndogo. Mwendesha baiskeli mmoja alivalia chapka ya mtindo wa Kirusi kichwani mwake na si kingine ila rangi ya kijani iliyomfunika kuanzia kichwani hadi miguuni,” jarida la AFP liliripoti.

Katika video ambazo zilipakiwa mitandaoni, na ambazo hatuwezi kukuonesha hapa kutokana na itifaki, waendesha baiskeli hao walionekana uchi kabisa na hawakujali utupu wao kuonekana hadharani.

"Tuko uchi kwenye moja ya njia kubwa za Amerika ya Kusini, kuonyesha kwamba tuko hatarini kwa nguvu, kutokana na vurugu za magari," mtumizi mmoja aliiambia AFP.

Aliongeza: "Harakati hizi zinaonyesha kwa jamii jinsi tulivyo muhimu. Kwa kutumia baiskeli kama njia yetu ya usafiri, tunaondoa magari barabarani ambayo yatakuwa yanachafua mazingira."