Mwalimu aliyemuua mwalimu mwenzake akutwa amejinyonga katika choo cha mahabusu

Mwalimu huyo alimvamia mwenzake darasani na kumuua akimgombanizia nafasi ya kufunza.

Muhtasari

• Baada ya kukiri kosa hilo, aliporudishwa mahabusu siku moja baadae mtuhumiwa huyo Samwel Abel alipatikana ananing’inia katika choo cha mahabusu.

Mwalimu aliyemuua mwenzake darasani ajiua pia.
Mwalimu aliyemuua mwenzake darasani ajiua pia.
Image: Screengrab//Global Tv Online

Mwalimu mmoja aliyekamatwa kwa kukiri kumuua mwalimu mwenzake shuleni apatikana amejitoa uhai kwa njia ya kikatili katika choo cha mahabusu.

Mwalimu huyo alikamatwa Machi 16 baada ya kumuua mwalimu mwenzake na baada ya kuhojiwa na vyombo vya dola, alikubali kutekeleza kitendo hicho na kuwekwa mahabusu akisubiri hukumu.

Mtuhukiwa huyo alikiri kumuua mwenzake kutokana na kugombania nafasi ya kufunza darasani.

Baada ya kukiri kosa hilo, aliporudishwa mahabusu siku moja baadae mtuhumiwa huyo Samwel Abel alipatikana ananing’inia katika choo cha mahabusu.

“Alichukua shati lake alilokuwa amevaa na kujitia kitanzi nalo. Juhudi zilifanyika za kumtoa na kumpeleka hospitali kwa sababu alikuwa hajafa lakini hatma yake ndio hivo, alikata Kamba…” kamanda wa polisi alidhibitisha kisa hicho.

Kamanda Jongo pia alisema kuwa visa vya watu kuuana kwa sababu ya kazi si vigeni kwani wengi huziendekeza tamaa zao katika kufanya hivyo wakiamini kwamba wenzao wanaofanikiwa mbele yao wanatumia ushirikina au vitu kama hivyo.

Alitoa rai kwa watu kuacha Imani za kishirikina na kuamini katika bidii na nyota ya Mungu kwani kunao wengine wanawaua wenzao katika hali ya kugombania madini pia.

“Tunajua kabisa riziki inatoka kwa Mungu lakini pia na juhudi. Hivi vitu vingine vya Imani za kishirikina tuache,” kamanda huyo alisema kwa kutoa wito kwa viongozi wa dini pia kufanya kazi katika kuelimisha jamii kumjua Mungu ili kuepuka visa kama hivyo ambavyo vimekithiri katika jamii nyingi.