Peru: Rais wa zamani mwenye umri wa miaka 84 kufungwa miaka 35 jela kwa ufisadi

Kuczynski, 84, anatuhumiwa kwa utakatishaji fedha na kuunda shirika la uhalifu ambalo linadaiwa kupokea dola milioni 12 (Ksh 1.6 bilioni) kwa njia ya kifisadi.

Muhtasari

• Baada ya kukaa miaka mitatu chini ya kifungo cha nyumbani aliruhusiwa kuachiliwa kwa masharti mnamo Aprili 2022.

• Mnamo 2018 alikua rais wa kwanza wa Amerika Kusini kujiuzulu kwa madai ya uhusiano na kashfa ya Odebrecht.

Kuczynski, rais wa zamani wa Peru.
Kuczynski, rais wa zamani wa Peru.
Image: BBC NEWS

Waendesha mashtaka nchini Peru siku ya Ijumaa waliomba rais wa zamani Pedro Pablo Kuczynski ahukumiwe kifungo cha miaka 35 jela kwa tuhuma za ufisadi zinazohusiana na kashfa kubwa ya Odebrecht, jarida la AFP limeripoti.

Kuczynski, 84, anatuhumiwa kwa utakatishaji fedha na kuunda shirika la uhalifu ambalo linadaiwa kupokea dola milioni 12 (Ksh 1.6 bilioni) kutoka kwa kampuni kubwa ya ujenzi ya Brazili Odebrecht kwa mashauriano ya siri.

Odebrecht, ambayo tangu wakati huo imebadilisha jina lake kuwa Nononor, ilikiri kulipa mamia ya mamilioni ya dola katika hongo kote Amerika Kusini ili kupata kandarasi kubwa za kazi za umma.

Inadaiwa Kuczynski alitumia kampuni zake za ushauri wa kifedha kushirikiana na Odebrecht.

"Yeye ni mtulivu kabisa, ana imani hali hiyo itatatuliwa na kwamba hakuna mtu anayeweza kumhusisha na vitendo vyovyote vya ufisadi," wakili wa rais wa zamani Julio Mindolo aliambia kituo cha redio cha RPP.

Mamlaka imekuwa ikichunguza kesi dhidi ya Kuczynski kwa miaka mitano. Baada ya kukaa miaka mitatu chini ya kifungo cha nyumbani aliruhusiwa kuachiliwa kwa masharti mnamo Aprili 2022.

Mindolo alikanusha kuwa rais wa zamani Alejandro Toledo alimshtaki mteja wake katika ushahidi alioutoa kwa mahakama mapema wiki.

Toledo, ambaye alikuwa rais kuanzia 2001-06, anazuiliwa kabla ya kesi yake kuzuiliwa kufuatia kurejeshwa kwake kutoka Marekani mwezi uliopita na anakabiliwa na mashtaka ya rushwa kuhusiana na kashfa ya Odebrecht.

Kabla ya Kuczynski kuwa rais mwaka wa 2016, alikuwa waziri katika serikali ya Toledo.

Mnamo 2018 alikua rais wa kwanza wa Amerika Kusini kujiuzulu kwa madai ya uhusiano na kashfa ya Odebrecht.

Marais wengine wawili wa zamani wa Peru, Ollanta Humala (2011-2016) na Alan Garcia (2006-2011), pia wameshtakiwa kwa ufisadi kuhusiana na kesi ya Odebrecht.

Kesi ya Humala ilianza Februari wakati Garcia alijiua Aprili 2019 polisi walipofika nyumbani kwake kumkamata.