Nitasambaza silaha kwa Urusi - asema Julius Malema wa Afrika Kusini

EFF pia inaitaka Afrika Kusini kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Muhtasari
  • "Nitaenda zaidi ya urafiki na Urusi.Katika vita, nitaungana na Urusi na hata nitasambaza silaha,” Bw Malema alimwambia Stephen Sackur wa HARDtalk.
Julius Malema
Image: TWITTER// EFF

Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), chama cha tatu kwa ukubwa cha kisiasa nchini Afrika Kusini, amesema "atasambaza silaha kwa Urusi" kwa sababu Moscow iko "katika vita na ubeberu".

Katika mahojiano na BBC mjini Johannesburg, Julius Malema alisisitiza kuwa "Afrika Kusini ni mshirika wa Urusi" na kwamba msimamo wa serikali ya ANC wa kutojihusisha na siasa unahusu vita vya Ukraine pekee.

"Nitaenda zaidi ya urafiki na Urusi.Katika vita, nitaungana na Urusi na hata nitasambaza silaha,” Bw Malema alimwambia Stephen Sackur wa HARDtalk.

EFF pia inaitaka Afrika Kusini kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Mahakama ya ICC imetoa hati ya kukamatwa kwa Vladimir Putin kwa tuhuma za uhalifu wa kivita lakini Bw Malema ameahidi kuzuia jaribio lolote la kumkamata rais huyo wa Urusi iwapo atahudhuria mkutano wa kilele wa Brics mwezi ujao mjini Cape Town.

Bw Malema alitoa maoni hayo kufuatia mzozo wa kidiplomasia ambapo balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini alidai kuwa silaha na risasi zilipakiwa kwenye meli ya Urusi iliyotia nanga nchini humo Desemba mwaka jana.

Serikali ya Afrika Kusini imekana kuidhinisha usafirishaji wowote wa silaha kwenda Urusi.