Wasioonyesha uzalendo kuadhibiwa nchini Zimbabwe

Mabadiliko hayo yenye utata yalipitishwa kama sehemu ya mfululizo wa marekebisho ya Sheria ya Jinai.

Muhtasari
  • Mswada huo unaojulikana kama kifungu cha uzalendo cha Sheria ya Jinai kinalenga wale wanaodhuru "maslahi ya kitaifa ya Zimbabwe".

Bunge la Zimbabwe limepiga kura kuunga mkono mswada wenye utata wa kuwaadhibu raia kwa "vitendo visivyo vya kizalendo", ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini kubwa au hata adhabu ya kifo.

Wakosoaji wametaja hatua hiyo kama pigo kwa demokrasia.

Mswada huo unaojulikana kama kifungu cha uzalendo cha Sheria ya Jinai kinalenga wale wanaodhuru "maslahi ya kitaifa ya Zimbabwe".

Inajumuisha raia yeyote anayekutana na mwakilishi wa nchi ya kigeni kwa lengo la kuhimiza vikwazo dhidi ya Zimbabwe au kupindua serikali.

Maafisa wengi waandamizi wa serikali na makampuni yanayomilikiwa na serikali wako chini ya vikwazo vya Magharibi kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu,

Kwa muda mrefu wamelaumu upinzani kwa hili na wanataka kusitisha mikutano kati ya upinzani na maafisa wa kigeni.

Bunge lilipiga kura 99 kwa 17 kuunga mkono sheria hiyo - mojawapo ya utata mkubwa wa urais wa Emmerson Mnangagwa.

Sasa muswada huo utawasilishwa katika bunge la seneti kabla ya kutiwa saini kuwa sheria.

Wakosoaji wanasema sheria hiyo ni kinyume na katiba kwa vile itakiuka uhuru wa kujumuika na haki ya kujieleza.

Afisa wa upinzani aliambia BBC kwamba njia ya kukomesha vikwazo ni kuzingatia haki za binadamu, na sio kuharamisha ukosoaji.

Mabadiliko hayo yenye utata yalipitishwa kama sehemu ya mfululizo wa marekebisho ya Sheria ya Jinai.

Wabunge pia walipiga kura kuunga mkono hukumu za kima cha chini kwa ubakaji.