Wenza waliokuwa fungate wapotea baada ya nyumba kusombwa na mafuriko

Watu katikati mwa Ugiriki walikwama kwenye paa za nyumba zao baada ya mafuriko kuweka vijiji chini ya maji.

Muhtasari
  • Lakini nyumba katika eneo la mapumziko la Potistika, karibu na Mlima Pelion, ilisombwa na mafuriko Jumanne jioni, ripoti zilisema.

Wanandoa kutoka Austria waliokuwa kwenye fungate hawajulikani walipo nchini Ugiriki baada ya mvua kubwa kunyesha kusomba nyumba waliyokuwa wakiishi.

Huduma za dharura zimeiambia BBC kuwa wanawatafuta wanandoa hao na watu wengine kadhaa waliopotea.

Watu katikati mwa Ugiriki walikwama kwenye paa za nyumba zao baada ya mafuriko kuweka vijiji chini ya maji.

Zaidi ya watu kumi na wawili sasa wamethibitishwa kufariki tangu Kimbunga Daniel kilipopiga Ugiriki, Uturuki na Bulgaria wiki hii.

Inasemekana wanandoa hao wa Austria waliamua kujihifadhi ndani ya jumba walilokuwa wamekodisha kwa ajili ya fungate yao huku mvua kubwa ikinyesha katikati mwa Ugiriki.

Lakini nyumba katika eneo la mapumziko la Potistika, karibu na Mlima Pelion, ilisombwa na mafuriko Jumanne jioni, ripoti zilisema.

Kikosi cha Zimamoto cha Ugiriki kilisema kilikuwa na timu katika eneo hilo kuwatafuta watu waliopotea, wakiwemo wanandoa hao wa Austria.

Baadhi ya maeneo ya Ugiriki yalipata hadi 800mm (inchi 31.5) za mvua katika siku za hivi karibuni - zaidi ya inavyoonekana katika mwaka mmoja.

Eneo tambarare la Karditsa katikati mwa Ugiriki lilielezewa kuwa liligeuka kuwa "ziwa", huku vijiji vilivyo karibu na Palamas vikizama majini.

Kimbunga Daniel kimekuwa kikipiga Ugiriki, Uturuki na Bulgaria tangu Jumatatu, na zaidi ya watu kumi na wawili wameripotiwa kufariki.