Mafuriko Libya: Watu 5,300 wapoteza maisha huku kukiwa na wito wa msaada wa kibinadamu

Mto wa maji ya mafuriko unaofanana na tsunami ulipiga Derna Jumapili baada ya bwawa kupasuka wakati wa kimbunga Daniel.

Muhtasari

• Kumekuwa na wito wa kutaka msaada zaidi wa kibinadamu huku waathiriwa wakiwa wamefunikwa na mifuko ya miili.

Image: BBC

Zaidi ya watu 5,300 wanaaminika kufariki baada ya mafuriko katika mji wa Derna nchini Libya, afisa mmoja amesema.

"Bahari mara kwa mara inatupa maiti kadhaa," Hisham Chkiouat, waziri katika utawala wa mashariki mwa Libya alisema.

Kumekuwa na wito wa kutaka msaada zaidi wa kibinadamu huku waathiriwa wakiwa wamefunikwa na mifuko ya miili na wengine kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja.

Mto wa maji ya mafuriko unaofanana na tsunami ulipiga Derna Jumapili baada ya bwawa kupasuka wakati wa kimbunga Daniel.

Vikosi vya uokoaji vinachimba vifusi vya majengo yaliyoporomoka kwa matumaini ya kupata manusura - lakini matumaini yanafifia na idadi ya waliofariki bado inatarajiwa kuongezeka zaidi.

Maafisa wanasema takribani watu 10,000 hawajulikani walipo, huku watu 30,000 wakikadiriwa kuwa wameyahama makazi yao, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) nchini Libya lilisema Jumatano.

Vyumba vya kuhifadhia maiti na hospitali zimezidiwa na miili.

Daktari wa Libya Najib Tarhoni, ambaye amekuwa akifanya kazi katika hospitali karibu na Derna, alisema msaada zaidi unahitajika.