Dar es Salaam yapiga marufuku biashara za masaji na utingishaji makalio kwa vipusa

"Kwa mfano juzi mumeona kuna picha inasagaa ya masaji wadada wanatikisa makalio yao kwenye maji sijui nini ile wanatoa mapofu." RC Chalamila alisema.

Muhtasari

• RC Chalamila alitoa tamko lake kuhusu kuenea kwa vilabu vya starehe ambavyo vinapiga miziki ya kuleta kero.

Dar es Salaam wapiga marufuku masaji
Dar es Salaam wapiga marufuku masaji
Image: Facebook

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania Albert Chalamila amepiga marufuku biashara za kutoa huduma za masaji au ukandaji lakini pia mwenendo wa kina dada kutembea mitaani na katika sehemu za starehe wakitingisha makalio yao.

Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wakuu wa wilaya zote katika mkoa huo mkubwa nchini humo, Chalamila alilalamika vikali kwamba baadhi ya biashara hizo ingawa aina leseni za kuhudumu, lakini zimemomonyoa maadili mazuri ya raia wa taifa hilo ambao wengi ni wahafidhina.

“Ni kweli ni mifumo ya kutoa leseni ila wakati Fulani hamuangalii biashara ambayo inaweza kuwa na athari katika jamii zinazotuzunguka. Kwa mfano juzi mumeona kuna picha inasagaa ya masaji wadada wanatikisa makalio yao kwenye maji sijui nini ile wanatoa mapofu. Hili linahitaji wakuu wa wilaya, madubwasha yote ya aina hiyo ambayo yanakiuka misingi ya maadili tuliyo nayo, mkazifunge zile biashara haraka, na mkazifunge kweli,” RC Chalamila alisema.

Kando na kufungwa kwa madubwasha ya masaji na kutingisha makalio, RC Chalamila alitoa tamko lake kuhusu kuenea kwa vilabu vya starehe ambavyo vinapiga miziki ya kuleta kero.

“Lakini hali ya sasa na kelele imezidi. Lazima tuwafundishe kuondokana na ushamba. Kelele nyingi hizi kwenye baa ni ushamba. Tukawape elimu ya miziki yao iishie kwa waliofuata miziki. Sasa hivi watu wengi wanalalamika, lakini ukiangalia wale wenye baa wana leseni. Katika hili, wakuu wa wilaya tufanye vikao na wamiliki wa baa,” alisema RC Chalamila.

Hatua hii inafuatia ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya uongozi wa Nairobi kupitia kwa gavana Sakaja pia kutoa tangazo la kufungwa kwa baa ambazo zimo kwenye sehemu za makazi.

Sakaja alilazimika kuchukua hatua hiyo kufuatia malalamishi kutoka kwa baadhi ya wakazi wa maeneo ambako vilabu vilikuwa vinapiga miziki yenye kero usiku kucha na kuwanyima usingizi.