Ng'ombe 27 wauawa kwa kupigwa na radi kufuatia mvua kubwa za El Nino zinazoshuhudiwa

"Kumlika tochi Zaidi nikaona rundo la ng’ombe wamegongana. Sikuamini kinachoendelea,” alisema mkulima huyo kwa majonzi.

Muhtasari

• Mzee huyo alisema aliishiwa na nguvu na kujikokota kwenda kwa jirani kumtaarifu kwamba radi imeua ng’ombe wake.

Ng'ombe wauawa kwa kupigwa radi
Ng'ombe wauawa kwa kupigwa radi
Image: Screengrab

Mtu mmoja amefariki dunia na ng’ombe 27 pia wamekufa katika tukio la kupigwa radi katika Mkoa wa Rukwa nchini Tanzania.

Kaitka tukio la kwanza, mkulima mmoja alikuwa shambani na ng’ombe wake wawili wakati radi ilipompiga pamoja na ng’ombe wake hadi kufa majira ya saa mbili asubuhi.

Katika tukio lingine, ng’ombe 25 walifariki kwa kupigwa na radi wakiwa zizini usiku, tukio ambalo limezua tumbojoto katika jamii hiyo.

Kwa mujibu wa Ayo TV, mkuu wa wilaya ya Sumbawanga iliyoko katika mkoa huo wa Rukwa aliwataka wananchi kutokula nyama ya ng’ombe hao kwa kuwa bado uchunguzi wa kina ungali unaendelea.

Mmiliki wa ng’ombe hao 25 alisimulia jinsi alibaini kisa hicho;

“Nikiwa kwenye nyumba nikasikia mngurumo mkubwa mpaka mle ndani kukawa kwekundu. Nikafikiri ni simu kuangalia nikapata iko sawa nikasema ngoja niizime. Katika ile harakati nikasikia ng’ombe anakoroma. Basi ndio nikawa navaa buti nikamulika tochi na kuja kuingia hapo nikamkuta ng’ombe mkubwa amelala, kumlika Zaidi nikaona rundo la ng’ombe wamegongana. Sikuamini kinachoendelea,” alisema mkulima huyo kwa jina Jacobo Regius.

Mzee huyo alisema aliishiwa na nguvu na kujikokota kwenda kwa jirani kumtaarifu kwamba radi imeua ng’ombe wake.

Tukio hilo limehusishwa na mzua za masika za El Nino ambazo zinashuhudiwa katika maeneo mbali mbali kote Afrika,

Itakumbukwa mapema wiki jana, UN walitoa taarifa kwamba mvua za El Nino si za kupuuzwa huku wakitabiri kuwa huenda zikaendelea kunyesha hadi Aprili mwaka ujao.