Papa Francis ataka kuzikwa nje ya Vatican

Papa Francis ameamua kurahisisha pakubwa taratibu za mazishi ya papa kwa kuwa wa kwanza kuzikwa nje ya Vatican.

Muhtasari

•Kabla ya papa kuongoza Ibada ya Misa katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Francis alionekana kupona kutokana na ugonjwa wa mkamba.

•Francis amesema atakuwa tayari kujiuzulu - kama Benedict alivyofanya mwaka 2013 - ikiwa afya yake itakuwa mbaya sana.

Image: BBC

Papa Francis ameamua kurahisisha pakubwa taratibu za mazishi ya papa kwa kuwa wa kwanza kuzikwa nje ya Vatican katika zaidi ya karne moja.

Papa, ambaye anatimiza umri wa miaka 87 siku ya Jumapili, alifichua mipango ya mazishi yake katika mahojiano na televisheni ya N+ ya Mexico Jumanne jioni.

Katika mahojiano na mwandishi wa mtandao huo wa Vatican, Valentina Alazraki, yaliyorekodiwa kabla ya papa kuongoza Ibada ya Misa katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Francis alionekana kupona kutokana na ugonjwa wa mkamba.

Francis alisema kutokana na imani yake kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu, ameamua kuzikwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Maggiore lililopo Roma, ambako huwa anaenda kusali kabla na baada ya kila safari yake ya nje.

Mapapa wengi wamezikwa chini ya Basilica ya Mtakatifu Petro.

Papa wa mwisho kuzikwa nje ya Vatican alikuwa Leo XIII, aliyefariki mwaka 1903 na kuzikwa katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterani mjini Roma.

Francis amesema atakuwa tayari kujiuzulu - kama Benedict alivyofanya mwaka 2013 - ikiwa afya yake itakuwa mbaya sana, lakini pia anaamini kuwa kujiuzulu kwa papa kusiwe jambo la kawaida.

Alipoulizwa kuhusu afya yake, alisema: "Najisikia vizuri, najisikia vizuri".Ugonjwa wa mkamba ulimlazimu Francis kughairi safari ya Dubai mwezi huu ili kuhudhuria mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi wa COP28.

Alifanyiwa upasuaji mwezi Juni kurekebisha ngiri ya tumbo na inaonekana kuwa amepona kabisa kutokana na upasuaji huo.Alisema anatarajia kufanya safari tatu mwaka ujao, kwenda mahali fulani huko Polynesia, Ubelgiji, na nchi yake ya asili ya Argentina kwa ziara yake ya kwanza huko tangu kuchaguliwa kwake 2013.