Mwanajeshi wa zamani amdunga mkewe mshale jichoni kabla ya kumuibia pesa

Katika kisa hicho kilichotokea Januari 24 mwaka huu mwendo wa saa tano usiku, Ocaya anasemekana kumpiga mkewe kwa mshale huo kabla ya kupora KSh42,000 katika duka lake la Kamari.

Muhtasari

• Uchunguzi wa awali umefichua kuwa siku hiyo ya maafa, Ocaya na Onom David walikuwa wakicheza kamari katika duka la mwathiriwa, Apio Grace.

• Hata hivyo, Onom alishinda pesa zote, jambo ambalo halikumfurahisha Ocaya.

 

Jamaa akirusha mshale
Jamaa akirusha mshale
Image: BBC NEWS

Polisi nchini Uganda wanamsaka mwanajeshi mstaafu mwenye umri wa miaka 53 anayetuhumiwa kumshambulia mkewe na kumchoma mshale katika jicho lake la kulia kalba ya kumuibia.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka nchini humo, afisa huyo wa zamani kwa jina Owiny Patrick almaarufu Ocaya anashtakiwa kwa kumpiga mkewe, Apio Grace, kwenye jicho lake la kulia kwa upinde na mshale baada ya mzozo wa kucheza kamari.

Katika kisa hicho kilichotokea Januari 24 mwaka huu mwendo wa saa tano usiku, Ocaya anasemekana kumpiga mkewe kwa mshale huo kabla ya kupora KSh42,000 katika duka lake la Kamari.

Uchunguzi wa awali umefichua kuwa siku hiyo ya maafa, Ocaya na Onom David walikuwa wakicheza kamari katika duka la mwathiriwa, Apio Grace. Hata hivyo, Onom alishinda pesa zote, jambo ambalo halikumfurahisha Ocaya.

“Akiwa na wivu na hasira, Owiny alianzisha vita na Onom, akitaka kurejeshewa pesa zake, lakini mke aliingilia kati. Mshukiwa alichukua upinde na mshale, ili kumpiga Ongom David, lakini mkewe alipojaribu kumzuia, alielekeza upinde na mshale kuelekea kwa mkewe na kumpiga jicho la kulia. Alizidi kuiba Ugx 7m, kutoka kwa duka la mkewe na kutoweka nayo,” Msemaji wa Polisi wa Uganda Fred Enanga alinukuliwa.

Mwathiriwa alikimbizwa katika Hospitali ya Abim na baada ya hapo, alipewa rufaa ya Hospitali ya Lacor kwa usimamizi zaidi.

Kwa sasa yuko nje ya hatari. Hata hivyo, mshale huo ulipofusha jicho lake la kulia, baada ya kupenya kwenye tundu la jicho na kubaki pale.

 

"Wote mwathiriwa, watoto wake na jamii wametiwa kiwewe na shambulio hilo," Enanga anakariri kisa hicho.