155 wafa, zaidi ya 200 wajeruhiwa kwa mafuriko Tanzania

Waziri mkuu Kassim Majaliwa alieleza kuwa zaidi ya nyumba 10,000 sambamba barabara na reli nazo zimeathirika.

Muhtasari

• Serikali ilisema hali ya joto duniani imesababisha mvua ya El Nino ambayo imeleta mvua kubwa katika maeneo mengi nchini Tanzania.

Image: HISANI

Watu 155 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 230 kujeruhiwa nchini Tanzania kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo, amethibitisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo.

Aidha takribani watu 200,000 na zaidi ya kaya 51,000 zimeathirika huku miundombinu mbalimbali ikiharibika.

Akitoa taarifa ya mwenendo wa mabadiliko ya hali ya hewa, athari zake na hatua zinazochukuliwa na serikali bungeni leo, Waziri Mkuu amezitaka kamati zinazosimamia maafa kwenye ngazi za wilaya, mkoa na taifa kuchukua hatua za haraka pindi hali ya dharura inapojitokeza ili kupunguza athari.

Majaliwa alieleza kuwa zaidi ya nyumba 10,000 sambamba barabara na reli nazo zimeathirika.

Alisema hali ya joto duniani imesababisha mvua ya El Nino ambayo imeleta mvua kubwa katika maeneo mengi nchini.

''Hapa nchini, mwezi Oktoba hadi Desemba, mwaka jana kulikuwa na ongezeko kubwa la mvua ambapo jumla ya mililita 534.5 zilipimwa ikilinganishwa na mililita 227.2 kwa mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 135. Vilevile, ongezeko hilo la mvua kubwa limeshuhudiwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili 2024 na utabiri wa hali ya hewa unaonesha kuwa mvua za masika zitaendelea hadi mwezi Mei, 2024,” alisema Majaliwa huku akisema mvua za Januari mpaka Aprili zimekuwa na madhara.

Image: HISANI

Aliitaja baadhi ya mikoa iliyoathirika zaidi kuwa ni pamoja na Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya na Kigoma.

Mikoa mingine iliyopatwa na madhara ni; Arusha, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Kagera, Songwe, Rukwa, Manyara, Geita, Iringa na Dodoma.

Hata hivyo, ametoa pole kwa waathiriwa na ameshauri wananchi kuchukua tahadhari wanapopita kwenye barabara na sehemu zilizo na maji.

Wananchi wa maeneo mbalimbali wameiambia BBC kuwa , serikali inapaswa kusaidia familia zilizoathirika kwa chakula, vifaa tib ana malazi katika kipindi hichi.

Mkazi mmoja wa wilaya ya Siha, kaskazini mwa Tanzania amesema, "Sijawahi kuona aina hii ya mvua kabla iliyoleta majanga. Miaka ya nyuma tulikuwa na El Nino lakini haikuharibu nyumba zetu kama ilivyo sasa…

“ …leo sina kitu, Nyumba imeharibika, mali nazo zimeenda, mimea imeharibika lakini naona ni athari za mabadiliko ya tabia nchi lakini pia ukiangalia tumeharibu mazingira na tumekata miti mingi hivyo madhara lazima yatukute,” alisema mkazi huyo.