Iran yatangaza siku tano za maombolezo ya kifo cha rais wake

Bw Raisi alifariki dunia katika ajali ya helikopta eneo la milima kaskazini-magharibi mwa Iran.

Muhtasari

•Vyombo vya habari vya serikali vilithibitisha kuwa alifariki dunia baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka siku ya Jumapili.

Image: BBC

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ametangaza siku tano za maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa nchi hiyo, Ebrahim Raisi.

Bw Raisi alifariki dunia katika ajali ya helikopta eneo la milima kaskazini-magharibi mwa Iran, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian.

Vyombo vya habari vya serikali vilithibitisha kuwa alifariki dunia baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka siku ya Jumapili.

Ayatullah Khamenei alisema ametoa rambirambi zake "kwa watu wapenzi wa Iran".

Bw Raisi, mwenye umri wa miaka 63, alikuwa ametajwa kuwa mrithi wa kiongozi mkuu.

Vyombo vya habari vya serikali vilisema uchaguzi utafanyika tarehe 28 Juni ili kuchagua rais mpya.

Wakati huo huo, makamu wa Rais Mohammad Mokhber ameteuliwa kushika madaraka ya muda.

Baraza la mawaziri la Iran pia limemteua naibu waziri wa mambo ya nje Ali Bagheri Kani kuwa kaimu waziri wa mambo ya nje.