Baba mzazi wa mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novart, Paroko msaidizi wa Parokia ya Bugandika Elipidius Rwegoshora na Desideli Evarist ambaye ni mganga wa jadi ni miongoni mwa watu wanaoshikiliwa na polisi mkoani Kagera kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mtoto mwenye ualbino wa umri wa miaka miwili na nusu.
Taarifa ya polisi imesema, watuhumiwa hao walieleza namna walivyoshiriki katika tukio la mauaji ya mtoto Asimwe, tukio lililotokea mkoani humo.
Polisi imesema kwa kushirikiana na raia walifanya msako mkali hadi usiku wa kuamkia Jumatano Juni 19 na kuwakamata watuhumiwa tisa wakiwa na viungo vinavyodhaniwa kuwa vya mtoto huyo wakiwa wamevihifadhi katika vifungashio vya plastiki wakitafuta mteja.
Taarifa ya polisi inasema Paroko msaidizi, Elipidius Rwegoshora anadaiwa kumfuata na kumshawishi baba mzazi wa mtoto ili wafanye biashara ya viungo vya binadamu.
Pia anatuhumiwa kuwa ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zote za uganga.
Mtoto Asimwe alichukuliwa nyumbani kwao kaskazini magharibi mwa nchi hiyo katika kijiji cha Bulamula, kata ya Kamachumu, wilayani Muleba mkoani Kagera Mei 30 majira ya saa mbili usiku.
Baada ya tukio hili la mtoto Asiimwe, polisi mkoani Kagera wanasema wameimarisha ushirikiano na wananchi kupata taarifa za wahalifu kwa haraka na kuimarisha ulinzi kwa watu wenye ualbino.
‘Kwa Kagera hili ndiyo limetokea, lakini sidhani kama yanaweza kutokea matukio mengine ya namna hiyo kwa mkoa huu kwa sababu polisi ipo karibu sana na wananchi na imejikita sana kwa polisi jamii na ile miradi yake lakini, kata zote zina wagakuzi kata na askari kata na vikundi shirikishi, kwa ujumla wananchi wamaeneo haya wamejipanga vizuri kwa sasa’
Miaka kumi iliyopita, juhudi kubwa zilifanywa kukamata wahalifu na kutoa elimu kwa umma kukabiliana na mauaji haya ya kikatili. Mathalani mwanzoni mwa mwaka 2015, zaidi ya waganga wa jadi 200 walikamatwa, wakihusishwa na mauaji haya ya kinyama. Kuibuka kwa matukio haya mapya kunaashiria uhitaji tena kwa jamii na vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi na usalama wa watu wenye ualbino Tanzania.
Matukio ya namna hiyo pia yamekuwa yakiripotiwa katika nchi Jirani ya Malawi.