Mwandamanaji aliyekamatwa na polisi Uganda adai alinyanyaswa kimapenzi

Zaidi ya vijana 90 walikamatwa na wengine kushtakiwa kwa kuwa kero kwa umma.

Muhtasari

•Baadhi ya wale walioachiliwa kutoka kizuizini pia wameripotiwa wakisema walidhulumiwa kingono na kusababisha ukosoaji mkubwa.

Image: bbc

Mwanaharakati wa Uganda, mmoja wa makumi ya watu waliokamatwa wiki hii kwa kushiriki maandamano yaliyopigwa marufuku anadai alinyanyaswa kingono akiwa kizuizini, wakili wake amesema.

Zaidi ya vijana 90 walikamatwa na wengine kushtakiwa kwa kuwa kero kwa umma kufuatia maandamano ya kupinga ufisadi yaliyofanyika katika mji mkuu, Kampala.

Baadhi ya wale walioachiliwa kutoka kizuizini pia wameripotiwa wakisema walidhulumiwa kingono na kusababisha ukosoaji mkubwa. Hata hivyo, polisi walikanusha madai hayo.

Maandamano ya kupinga ufisadi yalifanyika kwa siku mbili Jumanne na Alhamisi licha ya onyo kutoka kwa Rais Yoweri Museveni kwamba waandamanaji "wanacheza na moto".

Waandamanaji hao wakichochewa na maandamano ya hivi majuzi ya kupinga Mswada tata Fedha 2024, nchini Kenya, walikuwa wakitaka kujiuzulu kwa spika wa bunge ambaye amekuwa akituhumiwa kwa ufisadi, jambo ambalo amelikanusha.

Lakini polisi wa kutuliza ghasia wa Uganda walisitisha haraka maandamano hayo, wakiwashika wanaharakati vijana kadhaa, akiwemo mtangazaji maarufu wa TV, na kukaweka nyuma ya lori.

Wengine wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali lakini idadi isiyojulikana bado inazuiliwa na polisi, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.