•"Katika kitendo cha kujilinda dhidi ya vitisho hivi, IDF linafanya mashambulizi kulenga maeneo ya ugaidi," msemaji wa IDF Daniel Hagari alisema.
•Katika taarifa, IDF ilisema Hezbollah "imerusha makombora zaidi ya 150 kutoka upande wa Lebanon kuelekea eneo la Israeli".
Jeshi la Israeli linasema kuwa ndege zake za kivita zinashambulia maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon baada ya kubaini makombora na maroketi yakirushwa kuelekea Israeli.
"Katika kitendo cha kujilinda dhidi ya vitisho hivi, IDF (Jeshi la Ulinzi la Israeli) linafanya mashambulizi kulenga maeneo ya ugaidi," msemaji wa IDF Daniel Hagari alisema.
Israeli ilisema raia wa Lebanon wameonywa kuondoka mara moja katika maeneo ambayo Hezbollah, kundi la Kiislamu la Shia linaloungwa mkono na Iran, lilikuwa likiendesha shughuli zake.
Muda mfupi baadaye, Hezbollah ilisema kuwa imeanzisha mashambulizi makubwa ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Israeli kujibu mauaji ya kamanda mkuu wa kijeshi wa kundi hilo yaliyotokea mwezi uliopita.
Katika maeneo ya kaskazini mwa Israeli ving'ora vya kuonya kuhusu roketi zinazoingia vilisikika mapema Jumapili.
Hakukuwa na ripoti zilizotolewa haraka kuhusu majeraha yoyote.
Katika taarifa, IDF ilisema Hezbollah "imerusha makombora zaidi ya 150 kutoka upande wa Lebanon kuelekea eneo la Israeli".
Wakati huo huo, Hezbollah imesema tayari imerusha zaidi ya roketi 320 za Katyusha, ikisema kuwa ilikuwa ikishambulia kambi 11 za kijeshi za Israeli.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alisema anaitisha mkutano wa dharura wa baraza lake la mawaziri la usalama.
Ofisi ya Bw Netanyahu ilisema waziri mkuu na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant walikuwa ndio "wanaosimamia hali inayoendelea" kutoka kituo cha kijeshi cha IDF huko Tel Aviv.
Wakati huo huo, Hezbollah ilisema katika taarifa yake kwamba mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Israeli ni kujibu "uchokozi wa kikatili wa Wazayuni, ambao ulipelekea kuuawa kwa shahidi... Fuad Shukr".
Kamanda mkuu wa kijeshi wa kundi la Shia aliuawa katika shambulizi la anga la Israeli katika mji mkuu wa Lebanon Beirut mwezi Julai.
Israeli imekuwa ikirushiana risasi na kundi la wanamgambo lenye makao yake nchini Lebanon tangu kuanza kwa vita Oktoba mwaka jana na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Hamas, kama Hezbollah, inaungwa mkono na Iran.