Bobi Wine aendelea kupata afueni baada ya kudaiwa kujeruhiwa na polisi

Kiongozi huyo wa NUP anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kuondoa vipande vya bomu la kutoa machozi.

Muhtasari

•Chama cha NUP kilisema kuwa mwanasiasa huyo alipigwa na bomu la kutoa machozi ambapo mwanzoni ilidhaniwa kuwa jeraha lake lilisababishwa na risasi.

•Uchunguzi utafanywa ili kufafanua ukweli, taarifa ya polisi ilisema.

Image: BBC

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine alijeruhiwa mguuni katika makabiliano na polisi, lakini chama chake kinasema anaendelea kupata nafuu hospitalini.

Chama cha (NUP) kinachoongozwa na Robert Kyagulanyi, kilisema kuwa mwanasiasa huyo nyota wa pop alipigwa na bomu la kutoa machozi - mwanzoni ilidhaniwa kuwa jeraha lake lilisababishwa na risasi.

Tukio hilo lilitokea wakati kiongozi huyo wa NUP akiwa njiani kuwatembelea mawakili wake siku ya Jumanne huko Bulindo, takriban kilomita 20 kaskazini mwa mji mkuu, Kampala.

Taarifa kutoka kwa polisi ilisema maafisa wa eneo hilo waliripoti kwamba kiongozi huyo wa upinzani alijikwaa wakati akiingia kwenye gari lake.

Awali, akaunti ya mtandao wa X ya Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, ilitoa taarifa hiyo kwa mara ya kwanza, akisema: "@HEBobiwine amepigwa risasi mguuni na polisi huko Bulindo."

Kanda za video zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mwanahabari Solomon Serwanjja, ambaye alikuwa katika eneo la tukio, akimuonyesha kiongozi huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 42 akisaidiwa kutoka kwenye jengo akiwa na jeraha lenye kutoka damu kwenye paja lake la kushoto.

Uchunguzi utafanywa ili kufafanua ukweli, taarifa ya polisi ilisema.

Kiongozi huyo wa NUP anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kuondoa vipande vya bomu la kutoa machozi, wataalam wa matibabu katika Hospitali ya Nsambya mjini Kampala, waliambia waandishi wa habari.