Mfungwa aliyehukumiwa kifo na kukaa jela muda mrefu zaidi aachiliwa kutoka gerezani

Uamuzi huo unahitimisha mojawapo ya kesi ndefu na maarufu za kisheria nchini Japani.

Muhtasari

•Iwao Hakamada, ambaye amekuwa akisubiri kunyongwa kwa zaidi ya nusu karne, alipatikana na hatia mwaka wa 1968 kwa kumuua bosi wake, mkewe na watoto wao wawili vijana.

Image: BBC

Mzee wa miaka 88 ambaye ndiye mfungwa aliyehukumiwa kifo kwa muda mrefu zaidi duniani ameachiliwa huru na mahakama ya Japan.

Iwao Hakamada, ambaye amekuwa akisubiri kunyongwa kwa zaidi ya nusu karne, alipatikana na hatia mwaka wa 1968 kwa kumuua bosi wake, mkewe na watoto wao wawili vijana.

Hivi majuzi alikubaliwa kesi yake kusikilizwa tena huku kukiwa na tuhuma kwamba wachunguzi wanaweza kuwa walimsingizia ushahidi uliosababisha ahukumiwe kwa mauaji ya watu wanne.

Uamuzi huo unahitimisha mojawapo ya kesi ndefu na maarufu za kisheria nchini Japani.

Mnamo mwaka wa 2014, Hakamada aliachiliwa kutoka jela na kuruhusiwa kusikilizwa tena na mahakama ya Japan, baada ya mawakili wa upande wa utetezi kuonyesha kuwa DNA kutoka kwa chembechembe za damu iliyopatikana kwenye nguo inayodaiwa kuvaliwa na muuaji haikulingana na yake.

Tangu wakati huo amekuwa akiishi chini ya uangalizi wa dada yake, kutokana na hali yake ya akili kuwa mbaya.

Kesi za muda mrefu za kisheria zilimaanisha kwamba ilichukua hadi mwaka jana kwa kesi hiyo kuanza tena - na hadi Alhamisi asubuhi kwa mahakama kutangaza kama Hakamada atafutiwa mashtaka, au atanyongwa.

Hakamada ni mfungwa wa tano tu katika hukumu ya kifo kupewa fursa ya kesi kusikilizwa upya katika historia ya baada ya vita nchini humo.