Sonko amlipia mwanamume aliyeiba Naivas faini ya Sh100,000

Muhtasari
  • Mahakama ilimtoza Alvin Chivondo faini ya Sh100,000 au kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kuiba bidhaa za thamani ya Sh3,165
  • Bidhaa hizo ni pamoja na mchele kilo 5, mafuta ya kula lita 5 na sukari kilo 2
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Image: HISANI

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amelipa faini aliyotozwa mwanamume aliyepatikana na hatia ya wizi wa duka kutoka kwa duka kuu la Naivas.

Mahakama ilimtoza Alvin Chivondo faini ya Sh100,000 au kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kuiba bidhaa za thamani ya Sh3,165.

Bidhaa hizo ni pamoja na mchele kilo 5, mafuta ya kula lita 5 na sukari kilo 2.

Sonko alisema kwamba alifanya uamuzi huo kama njia yake ya kawaida ya kuwafikia watu wenye matatizo.

"Wakenya wengi wanaishi katika maisha duni kutokana na janga la COVID-19, wengi watasema kwamba ni PR lakini napenda kusaidia watu, hilo limekuwa shauku yangu tangu nikiwa shule ya upili huko Kwale boys," Sonko alisema.

Aliongeza kuwa:

"Pia nimeahidi kumpa hisa ya chakula cha mwezi mmoja pamoja na kumpa kazi pia."

Sonko pia amewataka wapinzani kutoingiza siasa katika kesi ya Alvin, na kwamba hakulipa faini yake kutafuta hatua zozote za kisiasa.

Chivondo ndiye alikuwa gumzo nchini kufuatia uamuzi wa mahakama.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga alitoa wito wa kuachiliwa bila masharti kwa mshukiwa.

Katika tweet Jumatano, Raila alidai Chivondo aachiliwe bila masharti.

"Alvin Linus Chivondo aachiliwe bila masharti! Wahalifu sasa wanapata ahueni ya kufanya kampeni kwa uhuru, huku wahalifu wadogo wakifungwa jela," Raila alisema.