(VIDEO) Mwanaume ashtakiwa na kupigwa faini ya 100K kwa kuiba mafuta ya kupika, sukari, mchele

Muhtasari

• Alvin Chivondo, 21, alishtakiwa kwa kuiba lita tano za mafuta ya kupika, kilo mbili za sukari, mchele na majani chai vyote vinavyogharimu bei ya shilingi 3,165 pesa za Kenya.

Alvin Chivondo katika mahakama ya Milimani
Alvin Chivondo katika mahakama ya Milimani
Image: Screengrabs: yOUtUBE

Mwanaume mmoja mkaazi wa Nairobi alishtakiwa Jumatano katika mahakama kuu ya Milimani kwa kosa la kuiba mafuta ya kupika, sukari miongoni mwa bidhaa nyingine kutoka kwa duka la jumla la Naivas tawi la Moi Avenue kati kati mwa jiji la Nairobi.

Alvin Chivondo, 21, alishtakiwa kwa kuiba lita tano za mafuta ya kupika, kilo mbili za sukari, kilo 5 za mchele na majani chai vyote vinavyogharimu bei ya shilingi 3,165 pesa za Kenya.

Mahakama iliambiwa kwamba Chivondo aliingia kwenye duka hilo la jumla kama mteja wa kawaida na kuchagua bidhaa hizo ambapo alijaribu kutoka pasi na kulipia na hapo ndipo walinzi walimkamata.

Mwanaume huyo alikiri mashtaka yake ambapo aliagizwa kulipa faini ya elfu mia moja au kuenda jela mwaka mmoja, jaji wa mahakama hiyo, Wendy Kagendo alitoa hukumu.

Kitendo hiki kinajiri wakati ambapo wakenya wengi wanazidi kulilia kupanda kwa gharama ya maisha ambapo bidhaa kama vile gesi na mafuta ya kupika vinaongoza orodha ya bidhaa zilizopanda bei zaidi.