"Unadhalilisha mahakama!" Wakenya wamsuta Raila kwa kutoa amri kijana aliyeiba Naivas kuachiliwa huru

Muhtasari

• Raila atupiwa maneno kwa kusema kijana aliyeiba bidhaa kuachiliwa bila masharti.

• Wakenya wamsuta kwa kutoa amri kwa kuidhalilisha mahakama, wamtaka badala yake afidie faini ile.

Raila Odinga, Alvin Linus Chivondo
Raila Odinga, Alvin Linus Chivondo
Image: MAKTABA

Wakenya kutoka matabaka mbali mbali Jumatano walifurika katika mitandao ya kijamii kulalamikia hukumu iliyotolewa na mahakama kuu ya Milimani jijini Nairobi dhidi ya mwanaume mmoja aliyesemekana kuiba vyakula kutoka duka la jumla la Naivas.

Mwanaume huyo Alvin Chivondo, 21, alishtakiwa kwa kosa la kuiba bidhaa zenye thamani ya shilingi 3165 kutoka duka la Naivas tawi la Moi Avenue na kupigwa faini ya laki moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Adhabu hiyo iliwaghafilisha wakenya na wakafanya maandamano ya mitandaoni huku wakisema haki haijatendeka kwa kijana huyo kwa sababu pengine hakuwa na mtu wa kumsaidia.

Wakenya hao hao walimjia juu vikali kinara wa ODM Raila Odinga ambaye pia aliungana nao kuteta kuhusu hukumu hiyo.

Odinga alikuwa ametoa amri ya kijana huyo kuachiwa huru mara moja kwa kigezo kwamba wizi wake ni wa chakula tu tena cha pesa kidogo hali ya kuwa wezi wa mabilioni ya fedha za serikali wako huru kupiga kampeni.

Bila shaka, Odinga alikuwa na maana yake lakini Wakenya waliipokelea kwa hali changamano ambapo wengi walimkashfu kwa kutoa amri hiyo hali ya kuwa hana cheo chochote serikalini.

Wengine pia walimjia juu kwa kusema kwamba amri yake inaingilia uhuru wa mahakama kwani kijana mwenyewe alikiri mashtaka na hakuna vile anaweza achiwa huru bila kufidia makosa yake.

Walimtaka badala ya kutoa maneno matupu kama amri ili kuikanyagia chini mahakama, ni bora angeingia mfukoni ili kumlipia faini ya laki moja aliyopigwa na kuachiwa huru.

“Alvin Linus Chivondo aachiwe huru bila masharti!. Wahalifu sugu wanapata afueni ya kufanya kampeni kwa uhuru, huku wahalifu wadogo wakifungwa jela. Acha mahakama zipate vipaumbele vyao sawa, kwa mara moja, huwezi kumfunga mwanaume kwa kujaribu kulisha familia yake,” Odinga alitoa amri kupitia mitandao ya kijamii.

“Baba lakini hapa nimekataa. Sheria haina upendeleo wa mtu. Wakubwa kwa wadogo wote wafungwe. As for this one, lipia yeye fine na patia yeye kazi kisha sisitiza ata wezi wakubwa wafungwe,” aliamjibu John Maloba.

“Mimi ni mfuasi wako lakini kwa hili sikubaliani kabisa, hataachiliwa bila masharti. Hakuna sababu ya kuiba bora ujitoe wazi huko ulipe faini pamoja na kumpa kazi,” Abdikadir Mohamed alimtupia cheche.