Msichana wa miaka 4 adondokwa na machozi mahakamani akisimulia jinsi babake alivyomnajisi

Muhtasari

•Kisa hicho kilitokea miezi kadhaa baada ya mamake mtoto huyo kufariki kutokana na maradhi ambayo hayakujulikana.

•Upande wa mashtaka ulilazimika kuingilia kati baada ya msichana huyo kuwezwa na hisia kali alipomuona mshtakiwa kortini.

Mahakama
Mahakama

Msichana wa miaka minne alisimulia mahakama jinsi babake alivyomnajisi pindi tu walipofika nyumbani kutoka kutoka kanisani.

Mwanamume huyo aliyetambulishwa kama PO alimchukua bintiye kutoka kwa shangazi yake baada ya kanisa na kumpeleka nyumbani kwake ambako inadaiwa  alitenda kitendo hicho cha unyama na aibu.

Jumanne, Hakimu wa mahakama ya Kibera William Tulen pia alisikia kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo siku chache tu baada ya kukamilisha kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa ambalo halikutajwa.

Kisa hicho kilitokea miezi kadhaa baada ya mamake mtoto kufariki kutokana na maradhi ambayo hayakujulikana.

Mwanamume alipokuwa gerezani na mkewe kufariki, watoto walikuwa wakiishi katika nyumba moja ya watoto jijini Nairobi. Mhasiriwa alikuwa anakaa na shangazi yake.

Siku ambayo kosa lilifanyika, PO alikuwa amerudi kutoka kwa safari na kisha akaenda kwa dadake mdogo na kumchukua binti yake.

“Baba yangu alirudi kutoka safarini na kunidhulumu. Alinisababishia uchungu mwingi,” msichana huyo aliambia mahakama.

Upande wa mashtaka ulilazimika kuingilia kati baada ya msichana huyo kuwezwa na hisia kali alipomuona mshtakiwa kortini. Alilia na kusababisha kesi kuchelewa kwa muda.

Karatasi za mahakama zilifichua shangazi ambaye alikuwa akimbadilisha nguo mtoto huyo alibaini jambo lisilo la kawaida kwenye sehemu zake za siri.

Kulingana na karatasi ya mashtaka, PO alitenda kosa hilo mnamo Januari 16 katika kijiji cha Matuini katika kaunti ndogo ya Dagoretti, Nairobi.

Alishtakiwa kwa kufanya kitendo kichafu na mtoto kinyume na sheria.

Alikanusha mashtaka na ombi lake la dhamana lilikataliwa baada ya upande wa mashtaka kusema anaweza kumvuruga shahidi.

"Tunapinga mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana kwani anaweza kumuingilia shahidi ambaye ni binti yake wa kumzaa," mwendesha mashtaka alisema.

Tulen aliahirisha kesi hiyo na kuagiza iendelee Mei 9 kwa ajili ya kusikilizwa tena.