Mshukiwa wa mauaji ya mwanariadha Agnes Tirop anyimwa dhamana

Muhtasari

•Hakimu Reuben Nyakundi alisema wakati wa kumpa mshukiwa dhamana bado haujafika baada ya kutathmini maelezo ya kesi hiyo. 

•Tirop alipatikana amekufa mnamo Oktoba 13 katika nyumba yake huko Iten ambako aliishi na Rotich kama mpenzi wake.

Wanafamilia wa marehemu Agnes Tirop wakiongozwa na babake Vincent Tirop wakiwa nje ya Mahakama Kuu mjini Eldoret Mei 11, 2022.
Wanafamilia wa marehemu Agnes Tirop wakiongozwa na babake Vincent Tirop wakiwa nje ya Mahakama Kuu mjini Eldoret Mei 11, 2022.
Image: MATHEWS NDANYI

Mahakama Kuu ya Eldoret imemnyima dhamana mshukiwa mkuu wa mauaji ya mwanariadha Agnes Tirop,  Ibrahim Kipkemboi Rotich.

Mnamo Jumatano Hakimu Reuben Nyakundi alisema wakati wa kumpa mshukiwa dhamana bado haujafika baada ya kutathmini maelezo ya kesi hiyo. 

Nyakundi alitaja mienendo ya mshukiwa wakati wa mauaji hayo ndio sababu kuu kwa nini haikuwa sahihi kumpatia dhamana.

"Ombi la bondi linaweza kukaguliwa baadaye lakini kwa sasa mshtakiwa atasalia rumande", Nyakundi alisema. 

Aliagiza kwamba kongamano la awali la kesi hiyo lifanyike tarehe 12 Juni 2022.

Katika uamuzi wake Nyakundi pia alibainisha kuwa mahakama ilizingatia usalama wa mshtakiwa katika uamuzi wa kumnyima dhamana.

 Jaji pia alibainisha kuwa Rotich alikuwa mtu asiyejulikana kwa sababu kwake hakukujulikana vizuri.

Ndugu wa mwanariadha huyo wakiongozwa na babake Vincent Tirop walikuwepo.

"Tunatumai kwamba hatimaye haki itatendeka kwa binti yangu", Mzee Tirop alisema. 

Rotich amekana kumuua Tirop mnamo Oktoba 12 katika eneo la Rural Estate katika mji wa Iten.

Rotich kupitia kwa wakili wake Ngige Ngugi alikuwa ametuma maombi ya kuachiliwa kwa bondi huku kesi ikiendelea. 

Hata hivyo, Wakili wa Serikali David Fedha aliwasilisha hati ya kiapo kupinga maombi hayo ya bondi.

 Mwaka jana Rotich alichukuliwa vipimo vya kidaktari na akapatikana anafaa kujibu mashtaka ya mauaji hayo. 

Tirop alipatikana amekufa mnamo Oktoba 13 katika nyumba yake huko Iten ambako aliishi na Rotich kama mpenzi wake. 

Uchunguzi wa maiti kwenye mwili ulifichua kuwa alifariki baada ya kudungwa kisu shingoni na kupigwa na kitu butu kichwani.