Mwanamke na dadake wazuiliwa baada ya mumewe kudungwa kisu hadi kufa

Muhtasari

•Polisi wameruhusiwa kumzuilia mwanamke, dadake na rafiki yao kwa siku 14 huku wakiendeleza uchunguzi zaidia wa mauaji ya mumewe.

•Afisa mpelelezi aliambia mahakama kuwa alihitaji muda zaidi kukamilisha uchunguzi ili kubaini kilichopeleka tukio hilo.

Maximilla Moraa na Nasma Blume katika Kibera law courts
Maximilla Moraa na Nasma Blume katika Kibera law courts
Image: CLAUSE MASIKA

Mahakama imewaruhusu polisi kumzuilia mwanamke, dadake na rafiki yao kwa siku 14 huku wakiendeleza uchunguzi zaidia wa mauaji ya mumewe.

Hakimu Derrick Kuto wa mahakama ya Kibera  aliamuru Sarah Rukia, Maximilla Moraa na Nasma Blume wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Kabete.

Mpelelezi wa polisi Fred Ambasa aliambia mahakama washukiwa hao walikamatwa Mei 7 kufuatia kisa cha mauaji kilichotokea mtaa wa Muthangari, kaunti ya Nairobi.

Taarifa ya mauaji hayo iliandikishwa katika kituo cha polisi cha Muthangari ambapo iliripotiwa kuwa marehemu alidungwa kisu hadi kufa baada ya ugomvi mdogo na mkewe.

Afisa wa upelelezi aliiambia mahakama kuwa dada wa mke wa marehemu aliripoti kuwa shemeji yake alidungwa kisu na kukutwa sakafuni akiwa amefariki.

Mahakama ilisikia kwamba mwanamke huyo (shahidi) alikimbia hadi kwenye nyumba hiyo ambapo alimkuta mwili wa marehemu ukivuja damu upande wa kushoto wa kifua huku ukiwa umelala sakafuni.

"Polisi walikimbia katika eneo la tukio na kubaini kuwa washtakiwa watatu walikuwa katika nyumba moja wakati kosa hilo lilipotekelezwa," mahakama ilisikiza.

Sarah Rukia katika Kibera law courts
Sarah Rukia katika Kibera law courts
Image: CLAUSE MASIKA

Afisa huyo aliambia mahakama kuwa alihitaji muda zaidi kukamilisha uchunguzi ili kubaini kilichopeleka tukio hilo.

“Ninahitaji ripoti ya uchunguzi wa maiti kutoka kwa daktari ili kubaini chanzo cha kifo. Ninahitaji mashahidi kurekodi taarifa zao na uchunguzi wa kiakili ufanywe pia,” alimwambia hakimu mkuu Kuto.

Aidha afisa wa upelelezi aliambia mahakama kuwa alihitaji siku 15 kumzuilia mlalamikiwa katika kituo cha polisi cha Kabete ili kukamilisha uchunguzi wake.

Alisema iwapo mshtakiwa ataachiwa huru, kuna uwezekano wa kuharibu ushahidi na wakati huo huo kutoroka mahakamani. 

Mwendesha Mashtaka Allan Mogere aliitaka mahakama kuzingatia maombi ya afisa wa upelelezi ili uchunguzi wa kina ufanywe.