Maafisa 8 wa kaunti ya Kericho wahukumiwa kwa kosa la ufisadi

Muhtasari

• Peter Koskey, Lillian Chepkoech, John Kimutai, Japheth Kipngeno, Joash Chirchir, Stanley Cheruiyot, Charles Mabwai, Aaron Njoroge na Jawlink Logistics Limited walipatikana na hatia  kwa kutoa zabuni ya ujenzi wa barabara ya Sh5.6 Milioni bila kuzingatia sheria.

• Washtakiwa hao walikabiliwa na mashtaka tisa ya tuhuma mbalimbali za rushwa.

• Koskey amehukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni 1.3 au kifungo cha miaka minane jela. 

Viongozi wanane wa Serikali ya Kaunti ya Kericho walipatikana na hatia kwa mashtaka tisa ya ufisadi mnamo Juni 2, 2022. Picha: EACC
Viongozi wanane wa Serikali ya Kaunti ya Kericho walipatikana na hatia kwa mashtaka tisa ya ufisadi mnamo Juni 2, 2022. Picha: EACC

Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Kericho siku ya Jumanne iliwahukumu maafisa wanane wa zamani wa kaunti ya Kericho waliopatikana na hatia ya ufisadi. 

Peter Koskey, Lillian Chepkoech, John Kimutai, Japheth Kipngeno, Joash Chirchir, Stanley Cheruiyot, Charles Mabwai, Aaron Njoroge na Jawlink Logistics Limited walipatikana na hatia siku ya Ijumaa kwa kutoa zabuni ya ujenzi wa barabara ya Sh5.6 Milioni bila kuzingatia sheria. 

Washtakiwa hao walikabiliwa na mashtaka tisa ya tuhuma mbalimbali za rushwa. Koskey amehukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni 1.3 au kifungo cha miaka minane jela. 

Alipatikana na hatia kwa makosa matatu ya ufisadi likiwemo la kutofuata kwa hiari utaratibu wa ununuzi na kutoa zabuni kwa Jawlink kwa njia ya moja kwa moja bila kufuata miongozo sahihi ya ununuzi. Chepkoech, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jawlink aliondolewa lawana kwa kosa la nne. 

"Mnamo Aprili 10, 2016, ukiwa Mkaguzi wa Barabara wa Kaunti ya Kericho, ulikosa kimakusudi kufichua nia yako ya kibinafsi kama Mkurugenzi wa Jawlink Logistics," ilisoma stakabadhi ya mashtaka ya sehemu ya shtaka la nne. 

Alihukumiwa kwa makosa ya tano, sita, saba na nane. Chepkoech atatozwa faini ya Shilingi milioni 10.5 milioni au kifungo cha miaka 10 jela. 

“Kosa la tano, mshitakiwa wa pili akiwa amepatikana na hatia chini ya kifungu cha 42(3) kikisomwa na 48(1) cha ACECA anatozwa faini ya Shilingi 500,000 au kifungo cha miaka mitatu jela na kwa mujibu wa kifungu cha 48(1)(b) na 48(2). )(a) ya ACECA, baada ya kupokea Shilingi 3,807,899.90 anatozwa faini ya lazima mara mbili ya kiasi kilichopokelewa, ambayo ni Shilingi 7,615,799.80 au kifungo cha miaka mitatu jela,” Mahakama iliamua. 

Katika makosa sita, saba na nane, Chepkoech alipatikana na hatia kwa pamoja na Kimutai na Kipngienoh. Walipigwa faini ya Shilingi milioni 2.4 kila mmoja au kifungo cha miaka minne jela. Chirchir, Cheruiyot, Mambwai na Njoroge walipatikana na hatia ya kukosa kufuata utaratibu wa ununuzi na kutoa zabuni hiyo kwa Jawlink mnamo Machi 9, 2016. Kwa makosa hayo, Hakimu Mkuu S M Mokua aliwapiga faini ya shilingi 300,000 kila mmoja au kifungo cha miaka miwili jela.