Meneja ashtakiwa kwa kuiba Sh2m za kodi ya nyumba

Muhtasari
  • Alikanusha mashtaka hayo mbele ya mkuu wa Kibera, Electa Rihani na kuomba aachiliwe kwa dhamana
Meneja ashtakiwa kwa kuiba Sh2m za kodi ya nyumba
Image: CLAUSE MASIKA

Meneja msaidizi ambaye alikuwa akisimamia baadhi ya vyumba huko Karen, Rongai na Kitengela alishtakiwa Jumanne kwa kuiba Sh2 milioni zilizokuwa za kodi ya nyumba.

James Peter Muthoga Mureke alishtakiwa kwa kuiba pesa hizo kutoka kwa Tweya Investment Limited, kampuni iliyomwajiri.

Hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani inasema mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa tarehe tofauti kati ya Juni 6, 2018 na Mei 26, 2022, katika barabara ya Karen Triangle ndani ya Kaunti ya Nairobi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, mshtakiwa huyo anadaiwa kupokea kiasi hicho baada ya ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na mtaalamu kuonyesha fedha hizo hazipo.

Alikanusha mashtaka hayo mbele ya mkuu wa Kibera, Electa Rihani na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Awali, mshtakiwa huyo alidaiwa kujipatia Sh1.4 milioni lakini upande wa mashtaka ulitaka kurekebisha hati ya mashtaka ambapo kiasi hicho kiliongezwa hadi Sh2 milioni.

Kabla ya hapo, mtuhumiwa alipinga ombi la upande wa mashtaka la kutaka kubadilisha hati ya mashtaka lakini baadaye alikubali ombi hilo.

Hakimu alimwachilia kwa dhamana ya Sh500, 000 pesa taslimu na kuagiza kesi hiyo itajwe Juni 22.

Pia aliamuru mshtakiwa apewe maelezo ya shahidi na ushahidi wa maandishi ambao upande wa mashtaka utautegemea wakati wa kesi.