Polisi 4 kufikishwa mahakamani kwa madai ya kuua mshukiwa wa wizi

Muhtasari

• Koplo Joseph Ojode na Charles Kirimi na konstebo Bashir Ali na Henry Mutai walidaiwa kuhusika katika mauaji ya Wycliffe Owuor huko Kayole. 

• Maafisa hao, wote wakihudumu katika Kituo cha Polisi cha Kayole, walikamatwa Jumatatu na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Capitol Hill eneo la Kilimani. 

• Kukamatwa kwao kulifuatia mapendekezo ya afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji mnamo Mei 18, 2022.

Wycliffe Owuor alipokamatwa kwa wizi wa Shilingi milioni 72 katika benki. Picha: KWA HISANI
Wycliffe Owuor alipokamatwa kwa wizi wa Shilingi milioni 72 katika benki. Picha: KWA HISANI

Maafisa wanne wa polisi wanatarajiwa kushtakiwa katika mahakama ya Milimani kwa madai ya kumuua mwanamume mmoja huko Kayole, Nairobi. 

Koplo Joseph Ojode na Charles Kirimi na konstebo Bashir Ali na Henry Mutai walidaiwa kuhusika katika mauaji ya Wycliffe Owuor huko Kayole. 

Owuor alikuwa mmoja wa washukiwa wa wizi wa Shilingi milioni 72 katika mtambo wa ATM mtaani Nairobi West uliofanyika mwaka 2019.

 "Watakabiliwa na mashtaka ya mauaji kinyume na Kifungu cha 203 kama kilivyosomwa na Kifungu cha 204 cha kanuni za adhabu," ripoti ya polisi ilisema. 

Maafisa hao, wote wakihudumu katika Kituo cha Polisi cha Kayole, walikamatwa Jumatatu na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Capitol Hill eneo la Kilimani. 

Kukamatwa kwao kulifuatia mapendekezo ya afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji mnamo Mei 18, 2022.

"Hii ni kwa kuzingatia pendekezo la ODPP kupitia barua yao ya res odpp/cam/1/1/1778 ya tarehe 18 Mei 2022 na barua ya dig kps ref kps/dig/sec/leg/11/4/103 ya tarehe 23 Mei 2022 inayohusisha kifo cha Wycliffe Owour." 

Taarifa iliyotolewa na idara ya mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) mwaka wa 2020 ilionyesha kuwa Owuor aliuawa kwa kupigwa risasi mnamo Machi 24, 2020, baada ya makabiliano makali ya risasi na polisi. 

Owuor alikuwa nje kwa dhamana ya shilingi 50,000 wakati huo. Alishukiwa kuwa mpangaji mkuu wa wizi wa shilingi milioni 72 katika mtambo wa ATM kwa Benki ya Standard Chartered mnamo Septemba 6, 2019.