Mshukiwa wa kulawiti watoto hatimaye asafirishwa kwenda Uingereza kujibu mashtaka

Anthony Kamau anatuhumiwa kulawiti watoto nchini Uingereza na kutoroka kuja Kenya baada ya kupewa dhamana

Muhtasari

• Mshukiwa huyo amekuwa akiukwepa mkono wa sheria kwa zaidi ya miaka miwili tangu akimbilie nchini.

• Mlawiti huyo anaripotiwa kuwalawiti wasichana wenye umri chini ya miaka 11 kuanzia 2005

Mshukiwa wa ulawiti Anthony Kamau
Image: DCI//FACEBOOK

Mshukiwa wa ulawiti sugu nchini Kenya hatimaye amesafirishwa kwenda nchini Uingereza ili kujibu mashtaka ya ulawiti yanayomkumba humo.

Kulingana na taarifa kutoka kwa kitengo cha upelelezi wa jinai ha uhalifu DCI, mshukiwa huyo wa ulawiti kwa jina Anthony Kinuthia Kamau ambaye ni Mkenya alitoroka kutoka taifa hilo la mkoloni kuja nyumbani baada ya kudaiwa kufanya vitendo vya ulawiti na kuukwepa mkono wa sheria.

Wapelelezi wa Kenya wakishirikiana na wenzao kutoka Uingereza wamekuwa wakimtafuta kwa muda mrefu na wiki chache zilizopita Kamau alitiwa nguvuni na sasa DCI wamesema tayari ameshasafirishwa kuelekea Uingereza ili kujibu mashtaka dhidi yake.

Inasemekana Kamau aliwahi tiwa nguvuni mara kadhaa nchini Uingereza kwa kuwalawiti watoto na mara ya mwisho alipoachiliwa kwa dhamana alitoroka kuja kenya kama njia moja ya kukwepa kujibu mashtaka katika mahakama ya Uingereza.

“Kamau anatakikana katika Mahakama ya Chelmsford ya Uingereza na Ireland Kaskazini, kujibu mashtaka ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto. Mlawiti huyo anaripotiwa kuwalawiti wasichana wenye umri chini ya miaka 11 kuanzia 2005. Pia alishitakiwa kwa makosa manne ya kujihusisha na mapenzi bila ya kupenyeza na msichana mmoja na lingine la kushawishi msichana mdogo kufanya tendo la ndoa,” sehemu ya taarifa ya DCI ilisoma.

Mshukiwa huyo amekuwa akiukwepa mkono wa sheria kwa zaidi ya miaka miwili tangu akimbilie nchini. Alishtakiwa mnamo June 17 na kumfikisha mahakamani ambapo agizo la kumsafirisha kwenda Uingereza kujibu mashtaka lilitolewa.