Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kiholela Nakuru akamatwa

Evans Michori Kebwaro, alifuatwa hadi maficho yake Alhamisi alasiri eneo la Keroka, Kaunti ya Kisii, alikokuwa amejificha

Muhtasari

• Imethibitishwa mauaji yote yaliyolenga wanawake na yalifanywa wakati wa mchana, na miili ya wahasiriwa kupatikana katika chumba cha kulala.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi wamemkamata mshukiwa mkuu wa mauaji ya kiholela ambayo yametikisa eneo la Mawanga, Nakuru kaskazini siku za hivi majuzi.

Evans Michori Kebwaro, alifuatwa hadi maficho yake Alhamisi alasiri eneo la Keroka, Kaunti ya Kisii, alikokuwa amejificha mara baada ya maafisa wa upelelezi kuanzisha msako.

Baadaye aliwafichua washirika wake watano Julius Otieno, 27, Josphat Simiyu, 24, Dennis Mmbolo 25, Isaac Kinyanjui, 18 na Makhoha Wanjala, 25, ambao wote wamejumuishwa katika operesheni ya siri iliyoendeshwa Nakuru, na kikosi maalum cha maafisa wa upelelezi.

Polisi wamegundua kuwa mshukiwa si mageni kwa maisha ya jela na ana historia ya uhalifu, ambayo hapo awali alipatikana na hatia na alitumikia vifungo gerezani.

Haya yanajiri baada ya mkutano wa hadhi ya juu wa usalama ambao ulifanyika mjini Nakuru ukiongozwa na waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i, kufuatia agizo la rais.

Imethibitishwa mauaji yote yaliyolenga wanawake na yalifanywa wakati wa mchana, na miili ya wahasiriwa kupatikana katika chumba cha kulala baada ya kuchomwa moto. Washukiwa hao waliletwa Nairobi kwa uchunguzi zaidi na maafisa wa DCI.